Wajukuu wa Samia kutangaza mafanikio ya Rais

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewateua wasanii wafupi wakiongozwa na Tausi Degela, Pimbi na Hamisi, kwa lengo la kusaidia kutoa elimu na kutangaza mafanikio makubwa ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema kuwa uteuzi huo ni sehemu ya mkakati wa mkoa kuhakikisha kila kundi katika jamii linashiriki kikamilifu katika maendeleo na kueneza taarifa sahihi kuhusu kazi zinazofanywa na serikali.
“Sisi ni wajukuu wa Samia, na jukumu letu ni kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi juu ya mafanikio makubwa ya Rais wetu,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake, msanii Tausi Degela amesema kuwa ni wakati muafaka kwa watu wenye ulemavu kuacha kutumika vibaya mitaani na kuanza kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa kujitegemea.
“Tumepewa mikopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi. Ni muhimu sasa tujenge biashara zetu zitakazotupa kipato, na pia tutoa elimu kwa jamii kuwa ulemavu siyo ugonjwa,” amesema Tausi.
Naye msanii Pimbi alitoa wito kwa watu wenye ulemavu, hususan wafupi, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi na kupiga kura, kwani ni haki yao ya msingi.
“Tusijifiche wala kuogopa. Huu ni wakati wetu wa kuonekana na kushiriki kwenye maamuzi ya nchi,” amesisitiza Pimbi