Wakamata bangi kilo 110, wateketeza mashamba
KATAVI; Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani Katavi, imekamata kilogramu 110 za bangi na kuteketeza ekari tatu za mashamba ya bangi.
Hayo yameelezwa na ofisa Sheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya Denastus Mnyika, ambapo watuhumiwa wawili wamekamatwa kuhusika na usafirishaji wa kiasi hicho.
Ukamataji huo ulifanyika kufuatia operesheni iliyofanyika kuanzia Mei 17 -23, 2024 katika Kijiji cha Kafisha, Kata ya Ikola, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi. Watuhumiwa walikamatwa wakiwa wanasafirisha bangi hizo zilizokuwa zimewekwa ndani ya mifuko ya sandarusi.
Akizungumza baada ya taarifa hiyo Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ametoa wito kwa wananchi wote wa Wilaya ya Tanganyika kuhakikisha wanapambana kwa pamoja kutokomeza biashara na matumizi ya dawa za kulevya.