Wakazi zaidi ya 400 Ilemela kunufaika kliniki ya ardhi

MWANZA: ZAIDI ya wakazi wapatao 400 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wanatarajia kunufaika na  kliniki ya ardhi itakayodumu kwa siku tisa huku ikiwa limeanza tangu Januari 11,2024 katika viwanja vya halmashauri ya manispaa hiyo.

Akiongoza kliniki hiyo pamoja na jopo la  wataalam wa ardhi kutoka ofisi yake kwa kushirikiana na wataalam wa ardhi katika Manispaa ya Ilemela Kamishna msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mwanza, Happyness Mtutwa amesema kuwa wanaendesha kiliniki hiyo ikiwa ni maelekezo ya Wizara ya Ardhi kuhakikisha wanawafuata  wananchi walipo na  kuwapa huduma kwa urahisi kwa huduma zote zinazohusu masuala ya ardhi.

“Tunaendela kutoa elimu kuhusiana na masuala yote yanayohusu sekta ya ardhi lakini pia tunatatua migogoro ,tunapokea malalamiko mbalimbali kikubwa sana tunatatoa hati pia tuna huduma ya ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa wale ambao bado hawajalipia”….Alisema

Advertisement

Aidha  katika hatua nyingine Mtutwa ametoa rai kwa wakazi wa Manispaa ya Ilemela na wakazi wa Mkoa Mwanza kiujumla kutumia fursa hiyo vizuri kwani wamejipanga vyema wakiwa na timu nzima ya wataalam ili waweze kuondokana na kero mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi ikiwemo migogoro.

Charles Theodory Mkazi wa Kata ya Kitangiri wilayani Ilemela ni mmoja kati ya wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo kwaajili ya kufuatilia hati ya kiwanja chake  kilichopo kata ya Nyamhongolo  kwa upande wake ametoa pongezi kwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi pamoja na wizara kwa ujumla kwa kuja na zoezi hilo huku akitoa wito kwa mamlaka husika kuboresha zaidi zoezi la kliniki hiyo kwa kuwafikia watu wengi haswa waliopo pembezoni mwa mji.

Naye Anthony Paul Mkazi wa Kata ya  Shibula ambaye alifika katika kliniki hiyo kwa siku ya kwanza kwa lengo la kutoa kero yake ya masula ya ardhi amesema kuwa  zoezi hilo ni zuri huku akitoa ushauri kwa mamlaka husika kuboresha zaidi kwa kuwafuata wananchi katika mitaa yao kwani kuna baadhi wa watu wanashindwa kuifuata huduma hiyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa pesa ya nauli .