Wakili Ambindilwe arejea kwa kishindo TLS Kanda ya Iringa

WAKILI Moses Ambindilwe ameibuka kidedea kwa ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society – TLS) chapta ya Iringa, baada ya kushinda nafasi ya Mwenyekiti bila kupingwa na kupata kura zote 45 zilizopigwa.

Ushindi wake atakaoutumikia kwa miaka mitatu umebeba ujumbe mzito wa kuimarika kwa TLS kanda ya Iringa, ambapo katika salamu zake za shukrani, Ambindilwe alisema:

“Uhai wa TLS sio kwamba umerudi tu, bali umerudi kwa kasi ya ajabu. Mwitikio huu unatupa matumaini sisi viongozi.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, kulikuwa na ushindani mkali ambapo Jessey Mwamgiga aliibuka mshindi kwa kupata kura 19, akiwashinda Emmanuel Chengula aliyepata kura 16 na Vedasto Chonya aliyepata kura 10.

Uchaguzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa haki jinai wakiwemo maofisa wa TAKUKURU, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo na Mahakama Kuu, pamoja na wawakilishi kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RCO).

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Ambindilwe aliahidi kuendeleza mafanikio yaliyokwisha kupatikana, yakiwemo ya utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo, kuendeleza mfuko wa kijamii unaowasaidia wanachama katika nyakati za furaha na majonzi, pamoja na kuimarisha mshikamano si tu miongoni mwa wanachama wa TLS, bali pia kati ya chama na wadau wote wa mahakama kupitia ushirikiano wa kitaalamu na shughuli za kijamii.

Akijibu hoja ya “No Reforms No Elections,” Ambindilwe alisisitiza kuwa “Kwa mujibu wa sheria, ni Tume Huru ya Uchaguzi pekee yenye mamlaka ya kuzuia au kuahirisha uchaguzi. Wengine wanaotaka kufanya hivyo wanataka kulifanya jambo hilo kisiasa badala ya kisheria.”

Makamu wa Rais wa TLS Taifa, Wakili Laetitia Ntagazwa, aliwaasa mawakili kujiunga na TLS na kushiriki kikamilifu katika shughuli zake.

Akiweka wazi changamoto zinazowakabili wanasheria, alisema baadhi ya watendaji wa mahakama huwapuuza mawakili na wakati mwingine kuwavunjia heshima mbele ya wateja wao.

“Kuna wakati hakimu au jaji anaweza kumtisha wakili mbele ya mteja wake. Hii haijengi mahusiano ya kuaminiana,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Iringa, Beatrice Nsana, alisema kila mmoja atimize wajibu wake kwa nafasi yake kwa ajili ya kulitumikia taifa, huku Kamanda wa TAKUKURU Mkoa, Victor Swela, akihaidi ushirikiano katika kusukuma mashauri ya jinai mahakamani ili haki ipatikane kwa wakati.

Akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa alisisitiza kuwa TLS ni mdau muhimu katika mfumo wa utoaji haki na utawala bora nchini.

“Mkutano huu ni muhimu kwa maendeleo ya TLS. Uchaguzi wenu unatarajiwa kuwa na maslahi mapana ya kanda na taifa. Naamini mtakaowqchagua hawatakuwa watu wa maslahi binafsi,” alisisitiza.

Alisema uchaguzi huo unapaswa kutumiwa kuonesha mwamko mpya ndani ya TLS Iringa, na kuwataka viongozi wapya kusimamia maadili, kutoa huduma kwa jamii na kulinda maslahi ya wanasheria wote wa kanda hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button