Wakili Ambindilwe atoa mafunzo ya haki na usuluhishi Isakalilo

“Wanaume wasisite kuripoti ukatili wowote unaofanywa dhidi yao. Mbele ya sheria, haki ni ya wote.”
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindilwe, wakati akitoa mafunzo kwa wajumbe wa Baraza Jipya la Kata ya Isakalilo yaliyolenga kuwawezesha katika usuluhishi wa migogoro ya ardhi na masuala ya haki za kijinsia.
Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria wa Manispaa ya Iringa pamoja na Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi, Wakili Ambindilwe alisisitiza kuwa sheria za nchi hazimfumbii macho mwanaume anapofanyiwa ukatili wa kimwili, kihisia au kiuchumi.
Alifafanua kuwa licha ya jamii nyingi kuona wanaume kama wahanga wasioeleweka wa ukatili wa majumbani, sheria zipo wazi: mwanaume ana haki ya kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili kama ilivyo kwa mwanamke.
Hata hivyo, alionesha kusikitishwa na ukweli kuwa wanaume wengi wanaogopa kuripoti ukatili wanaofanyiwa kwa kuhofia kubezwa, kudharauliwa au kutengwa na jamii.
Naye Mkaguzi wa Polisi, Elijah Bundala, kutoka Dawati la Jinsia alisema kuwa bado kuna changamoto kubwa ya wanaume kufungua kesi za ukatili wanaofanyiwa kutokana na mila, desturi na mitazamo ya kijamii.

“Mwanaume akisema kapigwa, anachekwa. Hili ni jambo linalohitaji mabadiliko ya kimtazamo,” alisema.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Manispaa ya Iringa, Robert Rumisha, alieleza jinsi mabaraza ya kata yalivyo na msaada mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi, jambo linalosaidia kupunguza mlundikano wa mashauri kwenye ngazi ya wilaya na mahakama.
Alisema migogoro mingi ya ardhi hutokana na mirathi isiyosimamiwa ipasavyo, ambapo wanandugu huingia katika migogoro inayodumu kwa miaka mingi.
Wakili Ambindilwe aliwakumbusha wajumbe wa Baraza kuwa kazi yao si kutoa maamuzi, bali ni kusuluhisha.
“Kazi yenu ni ya kujitolea, na hamtakiwi kuwatoza watu wanaofungua mashauri. Msitumie lugha ya ukali, na kumbukeni kwamba mashauri yoyote ya ardhi hayawezi kusikilizwa kwenye Baraza la Wilaya kama hayajapitia kwanza kwenye Baraza la Kata,” alifafanua.

Alisisitiza kuwa mabaraza ya kata yanaendeshwa kwa mujibu wa misingi ya sheria na nguzo za utawala bora kama vile uwajibikaji, usawa, na kuheshimu haki za binadamu.
Katika mada ya ustawi wa jamii, washiriki walikumbushwa kuhusu lengo kuu la kusaidia makundi yasiyojiweza – wanawake, wazee, watoto na watu wenye ulemavu – kwa kuwawezesha kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao, ikiwa ni pamoja na migogoro ya kifamilia kama ile ya wanandoa au malezi ya watoto.
Kwa upande wao wajumbe wa Baraza la Kata ya Isakalilo waliahidi kutumia elimu waliyoipata kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila ubaguzi wa kijinsia.



