Wakimbizi Sudan kukumbwa na baa la njaa

KHARTOUM : SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetoa onyo kuwa mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan wako hatarini kukumbwa na baa la njaa kufuatia ukosefu wa ufadhili wa misaada ya chakula.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Masuala ya Dharura wa WFP nchini humo, Shaun Hughes, hali hiyo inatishia kuathiri zaidi maisha ya wakimbizi, hasa ikizingatiwa kuwa mapigano hayo yamevuka mipaka na kuathiri pia nchi jirani zenye changamoto za usalama na upatikanaji wa chakula.
“Tunakabiliwa na mgogoro wa kikanda katika maeneo ambayo tayari yanakumbwa na uhaba wa chakula. Bila msaada wa haraka, huenda misaada ikasitishwa kabisa,” alisema Hughes.
WFP imesema huenda ikalazimika kusitisha misaada kwa wakimbizi walioko Misri, Ethiopia, Libya na Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na ukosefu wa fedha. SOMA: Sudan: Kambi ya wakimbizi Zamzam yashambuliwa
Tangu Aprili 2023, mapigano kati ya Jeshi la Sudan na kikundi cha waasi cha Rapid Support Forces (RSF) yamesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu, huku zaidi ya watu milioni 10 wakisalia wakimbizi wa ndani na wengine milioni nne wakikimbilia nchi jirani zikiwemo Chad, Misri na Sudan Kusini.



