Wakongomani wawe wamoja kutafuta amani ya kudumu DRC

JUHUDI mbalimbali za kuleta amani na utulivu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinaendelea katika sehemu mbalimbali za dunia kwa kuwakutanisha wadau wakuu katika mgogoro huo.
Kabla ya juhudi za sasa zinazoongozwa na Qatar na Marekani, Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) pamoja na jumuiya mbalimbali za kikanda kama vile Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilifanya juhudi kubwa ya kupata amani ya kudumu ikashindikana.
Katika kipindi chote hicho, viongozi ndani ya DRC hawakuwahi kuwa kitu kimoja ili kutafuta mchawi na hatimaye nchi kuachana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hata juhudi za sasa zinazoendelea ambazo zimeonesha mafanikio makubwa ya kufikiwa kwa amani ya kudumu, changamoto inayorudisha nyuma mafanikio hayo ni kukosekana kwa umoja baina ya Wakongomani wenyewe.
Ikiwa wananchi na viongozi wa DRC wataweza kusimama kwa pamoja na kuwa na kauli moja dhidi ya adui anayevuruga amani yao suala la kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita hivyo ni suala la jepesi na DRC ingepata amani ya kudumu ndani ya muda mfupi.
Kwa mfano, wakati Marekani chini ya Rais Donald Trump ikiwakutanisha mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za DRC na Rwanda na kusaini makubaliano ya awali ya kumaliza mgogoro huo, viongozi wa serikali ya DRC na waasi wameshindwa kuwa kitu kimoja na kuendelea na mgogoro.
Kwa hakika tunaungana na nchi, viongozi mbalimbali duniani ambao wanaongoza mazungumzo baina ya serikali ya DRC na waasi wa M23 ili kufikia makubaliano ya kumaliza vita ambavyo vinakaribia kufikisha nusu karne.
Katika hili tunaamini umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, wakati wajumbe wa serikali wanaendelea na mazungumzo na wale wa waasi Mjini Doha nchini Qatar kujaribu kufikia makubaliano ya kumaliza vita, umoja na mshikamano baina ya Wakongomani unahitajika sana.
Itakuwa vigumu sana kufikia makubaliano ya amani ya kudumu ikiwa hakutakuwa na subira kupisha mazungumzo yaendelee hadi utakapofikiwa muafaka utakaoleta amani na utulivu wa kudumu.
Tungependa viongozi wote wa DRC kuanzia wastaafu hadi waliopo madarakani kupanga na kuamua mustakabali wa nchi yao kwa kushirikiana pamoja kutatua changamoto iliyopo na kuhitimisha mgogoro huo uliogharimu maisha ya maelfu ya Wakongomani.
Sote tunafahamu kuwa amani inajengwa na mtu yeyote ama wa ndani ya nchi au nje ya nchi lakini ni ukweli usiopingika kuwa amani ya kweli na ya kudumu ni ile inayojengwa na wenyewe wanaohusika katika mgogoro huo.
Tunazipongeza nchi zote pamoja na viongozi wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika kusaka amani kwa lengo la kuwaletea na hatimaye kuwafanya watoto wa Mashariki wa DRC kulala usingizi mnono kwani watoto wote wa taifa hilo hawajui amani katika eneo la Mashariki mwa taifa lao.
Tunatoa rai kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kutochoka kushiriki katika kuisaka amani ya kudumu na hivyo kufanya juu chini kushawishi makundi yote ndani ya DRC kuwa sehemu ya makubaliano ya amani yatakayofikiwa ili kutorudishwa nyuma baada ya makubaliano kufikiwa.