Wakulima 20,000 kunufaika na skimu ya mkombozi

ZAIDI ya wananchi 20,000 wa tarafa ya Pawaga wilayani Iringa wataondokana na changamoto ya maji sambamba na kuwa na uhakika wa chakula pindi skimu ya umwagiliaji ya Mkombozi yenye ukubwa wa hekta 6000 itakapokamilika.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara, Kilimo na Mifugo imetembelea skimu hiyo na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa alisema skimu hiyo inayojengwa kwa zaidi ya Sh Bilioni 55 na serikali ya awamu ya sita kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itakamilika Februali, 2024.

Itakapokamilika alisema itasaidia upatikanaji wa maji katika kipindi chote cha kilimo na inatarajiwa kubadili maisha na mazingira ya kuishi ya wananchi wa tarafa hiyo na kuinua uchumi wa mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla.

“Mradi huu wa miezi 18, ulianza Septemba 1, 2022 na unategemewa kukamilika mwezi Februari mwakani. Mkandarasi yupo kazini anaendelea na ujenzi, ambao tayari umeshafikia asilimia 67,” alisema.

Alisema skimu hiyo ina jumla ya mifereji 20 itakayosambaza maji katika mashamba ya wakulima kipindi chote cha mwaka ikiwemo wakati wa kihangazi.

“Kwahiyo mradi huu utatoa uhakika wa kilimo cha mpunga kwa mwaka mzima na hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji wa chakula kitokanacho na zao hilo,” alisema.

Mbali na mafanikio hayo Mndolwa aliieleza kamati hiyo ya bunge kuwa moja ya changamoto inayowakabili ni mifugo kuingia eneo la ujenzi mara kwa mara hali inayokwamisha utekelezaji wa shughuli za mradi.

Akizungumuza kwa niaba ya kamati hiyo Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa Morogoro, Christine Ishengoma amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wakulima wa tarafa hiyo na kuwapelekea mradi mkubwa utakaoongeza tija katika kilimo chao.

“Niwaambie ndugu zangu wakulima mashamba haya ni yenu, yatumie ipasavyo kwa faida yenu na taifa kwa ujumla. Mradi huu unawapa nafasi ya kulima kilimo cha kisasa,” Ishengoma alisema.

Alisema kilimo cha umwagiliaji kina faida kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongeza mavuno kwa kuwa maji yanapatikana wakati wote na kinapunguza hatari ya ukame.

“Umwagiliaji unaweza kuruhusu kilimo cha mimea ambayo haikustawi vizuri katika hali ya asili ya mvua. Hii inaweza kuongeza aina ya mazao yanayolimwa na kuboresha lishe na kipato cha wakulima,” alisema.

Ishengoma alisema kamati yao inatarajia mradi huo utaongeza kipato cha wakulima na utapunguza utegemezi wa msimu wa mvua

Habari Zifananazo

Back to top button