Wakulima Kagera walia na mwekezaji kiwanda cha chai

BAADHI ya wakulima wa zao la chai Halmashauri ya Bukoba, mkoani Kagera wamemlalamikia mwekezaji wa kiwanda cha Kagera Tea Limited kwa kushidwa kutimiza wajibu wa kuwalipa madai yao ya ununuzi wa mazao ya chai Sh Milioni 65.
Wakulima hao walitoa malalamiko yao mbele ya Mkuu wa Mkoa Kagera, Albert Chalamila, alipotembelea kiwanda hicho, ili kusikiliza kero za wakulima.
Akizungumza Nestory Rugakingira, mkulima wa chai kutoka Kijiji Cha Kabale kata Karabagaine, alisema anashangazwa na mwekezaji kutoonekana kwa kipindi cha miaka miwili na alianza kulipa kwa kusuasua na sasa ni miezi 10, wakulima hawajaingizwa fedha zao.
“Tunashangaa sana, kila tukitaka kumuona anatuma mwakilishi, hatujui yuko wapi na taarifa inayosomwa hapa tunasikia anaenda Ulaya kutafuta masoko, hakuna siku wamekwama kuchukua chai yetu, lakini kama wanachukua chai kwa nini fedha hazilipwi? Familia zimetutenga hatuna maelewano,” alisema Rugakingira.
Naye Yahaya Salumu mkulima wa chai, alisema kwa sasa hata watoto wao wamegoma kushiriki shughuli za shamba kutokana na watoto kutonunuliwa mahitaji yao, baada ya kuchuma chai, hivyo wakiambiwa kusafisha mashamba ya chai wanadai fedha haionekani katika familia .
Adeventina Nestory Katibu wa Bodi ya Chai anayetokana na wakulima, alisema mwaka 2020 wakulima waliokuwa wanazalisha chai walikuwa 350, lakini wamepungua hadi kufikia 180, huku wengine wakiendelea kukata tamaaa na kushindwa kuzalisha chai wakishinikiza kulipwa fedha zao.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda, Resipicus Alfred na Antius Paulo kwa nyakati tofauti walimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa wanakidai kiwada hicho malimbikizo ya madeni mbalimbali tangu mwaka wa 2019 na hadi sasa hawajalipwa hata mishahara yao.
Akijibu hoja hizo, Meneja wa kiwanda, Salumu Joseph aliyemwakilisha mmiliki wa wa kiwanda, amekiri kuwepo changamoto kadhaa, ikiwemo madai hayo ya Sh Milioni 65 ya wakulima, pia na madai mbalimbali ya wafanyakazi.
Amezitaja sababu mbalimbali zilizosababisha hali hiyo hasa ni kushuka kwa bei ya chai kwenye masoko ya nje katika nchi zinazonunua chai hiyo, ambazo ni Kenya na Rwanda, hasa wakati wa ugonjwa wa Corona.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kutokana na changamoto hizo za madeni, baadhi ya wafanyakazi wametukimbia, hivyo nguvu kazi ya uzalishaji imepungua kwa sasa kiwango cha uzalishaji wa kiwanda ni chini ya asilimia 25 tofauti na hapo nyuma.
“Hivyo licha ya ugumu huu tunaendelea kufanya kila liwezekanalo, ili tulipe madeni haya yote kwa wakulima na wafanyakazi kwa upande wa wakulima mwezi Novemba mwaka jana tulipanga kuwa ifikapo Desemba tuweze kuwalipa, lakini hatukuweza kufanya hivyo, kwani tulikuwa hatujaikamilisha hizo fedha, ila ndani ya kipindi kifupi tutawalipa,” alisema Joseph.
Mkuwa Mkoa Albert Chalamila hakutoa majibu ya moja kwa moja kutokana na kutokumkuta mmiliki halisi, baada ya kupewa taarifa na Meneja kuwa yuko nje ya nchi, hivyo kuagiza ajitokeze ndani ya wiki moja.
“Ndugu zanguni wananchi wakulima na wafanyakazi, siwezi kuzungumza na mwakilishi, aje hapa mmiliki wa kiwanda hiki tuzungumze ni namna gani ya kutatua matatizo haya, niwasihi sana tuzidi kuwa watulivu, wakati tukiendelea kushughulikia masuala haya, lazima yapate ufumbuzi, ili kila mmoja apate stahiki zake, “alisema Chalamila.
Amesema pia ataunda Tume ya Uchunguzi kuhusu mkopo ulivyotumika baada ya mwekezaji huyo kuuchukua benki kwa lengo la kufufua kiwanda na kuongeza uzalisha.