Wakulima sasa mambo kidigitali

DAR ES SALAAM: Wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika nchini wanatarajiwa kunufaika na ongezeko la upatikanaji wa huduma za kidijitali na kifedha kupitia jukwaa la M-Kulima kufuatia Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC leo kusaini hati ya makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) yenye lengo la kuimarisha matumizi ya dijitali kwenye vyama vya ushirika nchini.

Ushirikiano huu unalenga kuongeza ufanisi, uwazi na ujumuishwaji wa kifedha ndani ya vyama vya ushirika kwa kuwezesha usajili wa kidijitali wa vyama na wanachama wake kupitia mfumo wa M-Kulima, pamoja na kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali na kifedha kwa wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika nchini.

Kama sehemu ya makubaliano hayo, Vodacom Tanzania pia imekabidhi Kompyuta Mpakato (Laptop) 35 kwa TCDC ili kurahisisha shughuli za kidijitali na kuimarisha uwezo wa taasisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema mpango huo unadhihirisha dhamira ya Vodacom ya kutumia teknolojia katika kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

“Vodacom, tunaamini kuwa teknolojia inaweza kuleta mabadiliko yenye maana kwa kuwaunganisha watu kwenye fursa zinazoboresha maisha yao. Kupitia ushirikiano huu na TCDC, tunaziwezesha taasisi za ushirika kwa kuwapatia zana za kidijitali na suluhu za kifedha kidijitali zitakazoongeza ufanisi wa kiutendaji, kuboresha uwazi na kuwawezesha wakulima kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa thamani katika kilimo,” alisema Kamando.

Kupitia mfumo wa M-Kulima, vyama vya ushirika vitapata huduma mbalimbali zikiwemo usajili wa wanachama, malipo ya fedha kidijitali, huduma za akiba na mikopo, pamoja na suluhisho nyingine za kidijitali zinazolenga kusaidia ukuaji endelevu na utoaji wa huduma bora.

Ushirikiano huu pia utajikita zaidi katika kuwajengea uwezo viongozi wa vyama vya ushirika kupitia programu za mafunzo, kuimarisha ujuzi wa kidijitali na uwezo wa kiutendaji.

Naye Msajili wa Vyama vya Ushirika na Afisa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dkt. Benson Ndiege, ameukaribisha ushirikiano huo na kusisitiza kuwa mabadiliko ya kidijitali ni muhimu katika kuimarisha vyama vya ushirika na kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama.

“Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kuviwezesha vyama vya ushirika nchini Tanzania kujiendesha kisasa. Kwa kutumia suluhisho za kidijitali, vyama vitaweza kuongeza ufanisi, kuimarisha uwajibikaji na kuleta thamani zaidi kwa wanachama, hususan wakulima ambao ni nguzo muhimu ya uchumi wetu,” alisema Dkt. Ndiege.

Ushirikiano huu unadhihirisha juhudi za pamoja za kuimarisha ujumuishwaji wa huduma za fedha kidijitali sambamba na kuharakisha kasi ya matumizi ya teknolojia ndani ya vyama vya ushirika nchini.

M-Kulima ni jukwaa la Kilimo kidijitali la Vodacom Tanzania lililoundwa maalumu kwa ajili ya kusaidia vyama vya ushirika (AMCOS na Vyama Vikuu vya Ushirika) pamoja na wakulima kufanya shughuli za kilimo kidijitali.

Huduma zinazopatikana katika jukwaa hili ni pamoja na usajili wa wakulima, kufanya malipo, ukusanyaji wa mazao, pamoja na upatikanaji wa huduma za kifedha ikiwemo mikopo, akiba, bima pamoja na uwekezaji. Jukwaa hilo pia linatarajia kuboresha uwazi na ufanisi wa kiutendaji, huku likichochea zaidi ujumuishaji wa kifedha na kuwezesha wakulima kutunza kumbukumbu kidijitali zinazowaunganisha na uchumi rasmi.

Hadi sasa, mfumo wa M-kulima umesajili wakulima zaidi ya 3.2 milioni na kuchakata malipo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 88 kwa zaidi ya wakulima 325,000, jambo linalodhihirisha ukuaji na matumizi mapana ya mfumo huo katika sekta ya kilimo nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button