Wakulima Shinyanga wanufaika na Amco’s

SHINYANGA: WAKULIMA 164,400 mkoani Shinyanga wamenufaika na huduma kupitia Vyama vya Msingi (Amco’s) huku vyama hivyo vikiendelea kuimarishwa zaidi na kupewa elimu ya mara kwa mara.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga Ibrahim Kakozi amesema hayo kwenye jukwaa la maendeleo ya ushirika lililofanyika mjini Kahama huku akieleza ushirika una wanachama zaidi ya 28,000.

Kakozi amesema vyama vya ushirika vinaendelea kuwa na mali zenye thamani ya mabilioni ya fedha lakini bado kuna changamoto za upungufu wa watendaji, uelewa mdogo wa baadhi ya wanachama na udhaifu wa nidhamu ya mikopo.
Kakozi ametoa wito wa kuimarishwa kwa matumizi ya mifumo rasmi ya malipo badala ya fedha taslimu ili kuongeza uwazi na kupunguza upotevu wa fedha katika minyororo ya biashara ya mazao.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) Emanuel Nyambi amesema sekta ya ushirika Mkoa wa Shinyanga imeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuongeza ajira, masoko na kipato cha wakulima.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro alisema ushirika ni nyenzo muhimu ya utekelezaji wa sera za maendeleo za Serikali katika kuinua uchumi wa wananchi hususan wakulima.

Mtatiro amesema Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa pamba na tumbaku nchini huku akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Serikali, vyama vya ushirika na wadau wa maendeleo.
Mtatiro amesema Serikali kupitia mfumo wa ushirika imeendelea kutoa ruzuku ya pembejeo ikiwemo mbolea na viuatilifu hatua iliyosaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima.



