Wakulima wa mikunde Kigoma walia na bei

KIGOMA: WAKULIMA wa mazao jamii ya mikunde mkoani Kigoma wameiomba serikali na wadau wa kilimo kuwasaidia suala la upatikanaji wa masoko ili kuendana na mpango wa serikali na wadau wa kilimo kufanya mazao hayo kuwa kilimo biashara.

Wakulima hao wametoa kilio chao  wilayani Uvinza mkoani Kigoma wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mikunde duniani maadhimisho ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Advertisement

Agness Gabriel mkulima wa mazao ya mikunde mkoani Kigoma

Mmoja wa  wakulima hao, Agness Gabriel kutoka Kijiji cha Kalenge Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma alisema baada ya kishiriki katika mpango wa kilimo bora chenye tija kwa kufuata maelekezo ya wataalam wamefanikiwa kuongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

Naye Samson Mathias Mkulima kiongozi kutoka Kijiji cha Mazungwe Uvinza amesema kuwa hawana masoko ya uhakika kulingana na uzalishaji ulioongezeka kwani hata wateja wanaowapata wamekuwa wakija na masharti yao ikiwemo kutumia vipimo vya mabakuli badala ya mizani za kawaida jambo ambalo linawanyonya kimaslahi.

Samson Mathias mkulima kiongozi mazao ya mikunde kijiji cha Mazungwe Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma

Akizungumza katika maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza mkoani Kigoma, Acland Kambili amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa mpango wa kuongeza uzalishaji katika mazao ya mikunde bado matumizi ya mazao hayo kwa wananchi wa kawaida yapo chini hivyo kutokuwa na faida kiuchumi kwa wakulima hao na kuwataka maafisa kilimo wa halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa kilimo kuwa na mipango ya kuwatafutia wakulima hao masoko ya uhakika ya mazao yao.

Acland Kambili – Kaimu DED Halmashauri ya Wilaya Uvinza.

Awali mratibu wa maadhimisho hayo Afisa Kilimo katika halmashauri ya wilaya Uvinza, Tuligwe Kaisi alisema kuwa mpango wa kuongeza uzalishaji wa mazao jamii ya mikunde unaotekelezwa na halmashauri kupitia FAO katika mpango wa Pamoja Kigoma (KJP) umekuwa na mafanikio makubwa ambapo pamoja na kuongeza uzalishaji pia wanaangalia suala la masoko kwa mazao hayo.

Tuligwe Kaisi Ofisa Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *