Wakulima walalamikia upimaji utamu wa miwa Kilombero

WAKULIMA wa miwa wilayani Kilombero mkoani Morogoro, wamelalamikia kukosa imani na Kiwanda cha Sukari Kilombero kwa jinsi wanavyopima kiwango cha utamu wa miwa wauzayo kiwandani hapo, ambayo hupewa malipo madogo kwa madai utamu uko kiwango cha chini.
Malalamiko hayo yametolewa leo wilayani hapa na wananchi wakulima wa miwa mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo akiendelea na ziara yake mkoani Morogoro ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM ,kukagua uhai wa chama na kukiimarisha ngazi ya mashina.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kilombero, Mbunge wa Kilombero, Abubakar Assenga, amesema changamoto kubwa ni mgogoro baina ya wakulima wa miwa na kiwanda cha Kilombero.
“Mgogoro mkubwa ni kiwango cha utamu wa mua (Sucrose), malipo ya mkulima anayekwenda kuuza miwa yake kiwandani hapo yanategemea utamu wa mua, sasa wakati kupima hakuna mkulima anayepewa fursa ya kujua bali anaambiwa utamu wa mua ni mdogo na malipo yanakuwa madogo,” amesema Assenga.
Amesema mgogoro huo ni wa muda mrefu na viongozi wengi wamepita, lakini tatizo liko palepale.
Akizungumzia kero na malalamiko hayo, Chongolo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kutengeneza utaratibu wa kukaa na Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Biashara(Amcos), viteue wakulima mmoja mmoja wafundishwe jinsi ya kufahamu upimaji wa kiwango cha utamu wa sukari, ili kuondoa manung’uniko yao.