Walimu wa hesabu kuandaa wanafunzi uchumi kidigitali

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari amewataka walimu wa hisabati ambao wana nafasi muhimu katika elimu ya sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati, kuchukua nafasi ya mbele katika kuandaa wanafunzi wao kwa uchumi wa kidijiti.

Aliyasema hayo wakati akiwasilisha mhadhara wa mwaka wa teknolojia ya mawasiliano na hisabati kwenye mkutano wa mwaka wa wataalamu wa hisabati nchini, unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki Mkwawa (MUCE) mjini Iringa.

Mkutano huo unaoandaliwa na Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), huwakutanisha wataalamu hao kutoka mikoa yote nchini kwa malengo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo na warsha kwa walimu wa hisabati ili kuongeza ujuzi na maarifa yao katika kufundisha somo hilo kwa ufanisi.

Dk Bakari alisema hesabu ni msingi wa sayansi na teknolojia, na katika ulimwengu unaobadilika haraka wa teknolojia, uchumi wa kidijiti unakuwa injini muhimu ya ukuaji wa kiuchumi.

Alisema kwa kutumia fursa zinazotolewa na teknolojia, walimu hao wanaweza kuboresha mbinu zao za kufundisha na kuwezesha wanafunzi wao kuwa washiriki wazuri katika uchumi huo unaokua kwa kasi.

“Unapooana matumizi ya akili bandia au teknolojia ya habari na mawasiliano au chochote kile kinachohusisha kanuni, ujue nyuma yake kuna hesabu,” alisema.

Dk Bakari alibainisha kuwa mapinduzi ya kidijiti yameleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu. Katika mazingira ya sasa, vifaa vya kufundishia kama vile kompyuta, programu za hisabati, na mifumo ya kujifunza mtandaoni vinatoa mbinu mpya na bora za kufundisha hisabati.

“Walimu wa hisabati wana fursa ya kujiendeleza na kutumia zana hizi za kidijiti ili kuwasaidia wanafunzi wao kuelewa na kupenda somo hili muhimu,” alisema.

Aliongeza kuwa walimu wanaoweza kutumia programu hizo kwa ufanisi wanaweza kusaidia wanafunzi wao kufikia viwango vya juu zaidi vya elimu na kuwa tayari kwa fursa za kiuchumi katika uchumi wa kidijiti.

Awali, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Deusdedit Rwehumbiza, alisema walimu wa hisabati wanapaswa kuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa wanafunzi wao wanapata maarifa hayo muhimu kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.

Akitoa mfano, Profesa Rwehumbiza alisema uchanganuzi wa data unahitaji uelewa wa hali ya juu wa takwimu, algebra, na hesabu, ambazo zote ni sehemu kuu za hisabati.

“Walimu na wanafunzi wanapaswa kuelekeza juhudi zao katika kuelewa matumizi ya hisabati katika maeneo hayo. Hii itawaandaa kwa soko la ajira linalobadilika na kuwawezesha kushindana katika uchumi wa kidijiti,” alisema.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Iringa, Hansi Mgaya, alisema serikali inatambua changamoto ambazo walimu wa hisabati wanakabiliana nazo toka ngazi ya chini hadi ya juu, ambazo zinakwamisha juhudi za kuingia katika uchumi kidijiti.

Ili kushughulikia changamoto hizo, Mgaya alisema serikali na wadau wengine wa elimu wanapaswa kuendelea kuwekeza katika kutoa mafunzo kwa walimu na kuboresha miundombinu ya teknolojia katika shule.

Pamoja na uwekezaji huo, Mgaya alisema serikali inapaswa kuanzisha utaratibu wa kutoa motisha kwa walimu wa hisabati na kuboresha mishahara yao ili kuwahamasisha kujituma zaidi katika elimu, utafiti, na ubunifu.

Mwenyekiti wa CHAHITA, Dk Said Sima, alisema mafunzo ya mara kwa mara na upatikanaji wa vifaa vya kisasa ni muhimu ili kuhakikisha kuwa walimu wa hisabati wanakuwa na uwezo wa kuingia katika uchumi wa kidijiti na kuwasaidia wanafunzi wao kufanya hivyo pia.

Akizungumzia umuhimu wa hesabu, Dk Sima alisema inatumiwa katika taaluma mbalimbali kama uhandisi, sayansi, teknolojia, uchumi, fedha na uhasibu, afya na tiba, mazingira, usafiri na usafirishaji, michezo, na biashara, na huchangia katika uchambuzi wa data, kubuni mifano, kufanya maamuzi, na kutatua matatizo kwa ufanisi.

Habari Zifananazo

Back to top button