WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza wametakiwa kuchukua mikopo sasa wakiwa katika utumishi ili kuanzisha miradi ya kiuchumi ambayo itawafanya kuwa na msingi wa maisha bora baada ya kustaafu.
Ofisa utumishi wa halmashauri hiyo, Acland Dominic Kambili amesema hayo katika kongamano la siku moja kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wa halmashauri hiyo iliyoandaliwa na Benki ya NMB ili kutoa suluhisho la huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo mikopo.
Kambili amesema kuwa fursa ya mikopo kwa watumishi wa umma wanapokuwa kwenye utumishi ni muhimu kwa ajili ya kuwaandalia maisha yao ya baadaye kwa kuanzisha miradi ambayo itakuwa ndiyo ngao yao baada ya kustaafu.
Ofisa utumishi wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza (katikati) akizungumza katika semina ya siku maalum ya walimu wa Halmashauri ya Qilaya Uvinza iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa ajili ya kutoa elimu ya masuluhisho ya huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo.
Amesema kuwa walimu wanapaswa kuchukua mikopo sasa kuanzisha miradi ya kiuchumi kwa kupata elimu ya uendeshaji miradi hiyo badala ya kuchukua mikopo kufanya anasa na kuwa balaa kwa watumishi hao na familia zao.
SOMA: Benki yazindua huduma maalum kwa wastaafu
Akifungua kongamano hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza, Fred Millanzi amesema kuwa mikopo iliyotolewa na benki hiyo kwa walimu na watumishi wa halmashauri hiyo imewezesha walimu hao kuanzisha miradi ya kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi, Restus Assenga akizungumza katika semina ya benki hiyo na walimu wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza maarufu kama Teacher’s Day unaoendelea nchini kueleza huduma za kifedha zinazoweza kuinua Maisha ya walimu hao kiuchumi.
SOMA: Benki yazindua akaunti ya mfugaji
Awali Meneja wa Kanda ya Magharibi wa benki hiyo, Restus Assenga akizungumza katika semina ya benki hiyo na walimu wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza amesema kuwa semina hiyo imelenga kutoa elimu ya fedha kwa wlimu hao lakini kutangaza fursa za masuluhisho ya huduma za fedha ambazo zinapatikana katika matawi ya benki hiyo.