Benki yazindua huduma maalum kwa wastaafu

Dar es Salaam: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua huduma maalum kwa ajili ya wastaafu inayofahamika kama “Akaunti ya Wastaafu” ama “Pensioners account” ikilenga kutoa huduma za kibenki zenye kutoa vipaumbele kwa kundi hilo la kijamii.

Kupitia huduma hiyo iliyozinduliwa mapema leo Ijumaa, jijini Dar es Salaam, pamoja na faida nyingine inatoa fursa ya mikopo mikubwa hadi milioni 300 kwa wastaafu, itakayolipwa kwa kipindi cha miaka 9 huku walengwa wakinufaika na ushauri wa kifedha na elimu ili kuwajengea maarifa na rasilimali wanazohitaji kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha zao na malengo yao ya kifedha.

Akiizungumzia zaidi huduma hiyo, Mkuu wa Idara ya Wateja wadogo na Wakubwa wa benki hiyo, Elibariki Masuke alisema imeangazia zaidi katika kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali za huduma za kifedha zinazokabili wastaafu nchini huku ikitoa mwanga wa kesho bora kwa kundi hilo kupitia upendeleo maalum wa kihuduma.

SOMA: Utalii matibabu, wagonjwa Sierra Leone kutibiwa JKCI 

“NBC imeamua kumuangalia kipekee mstaafu kwa sababu tunaelewa umuhimu wa kipindi cha kustaafu. Kustaafu sio tu mwisho wa kazi, ni mwanzo wa sura mpya yenye uhuru wa kifedha na usalama. Ni wakati ambapo tunapaswa kuhakikisha kwamba wastaafu wetu wanapata huduma za kifedha zilizoboreshwa ambazo zitawawezesha kustawi kifedha.’’

‘’Tunatambua changamoto ambazo wastaafu wanakabiliana nazo, na ndio maana NBC tumechukua hatua za kuboresha huduma zetu za kibenki ili kukidhi mahitaji ya wateja wetu walio katika makundi mbali mbali ya mahitaji.’’ Alisema.

Zaidi alitaja faida nyingine zinazoambatana na akaunti hiyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na makato ya ada ya kila mwezi huku upatikanaji wake ukirahisishwa kidigitali kwa njia ya simu yaani NBC Kiganjani, na pia kupitia msaada binafsi kutoka kwa wataalamu wa benki hiyo.

Akizungumzia mafunzo na elimu ya fedha kwa wastaafu, Meneja Bidhaa na Mauzo wa benki ya NBC, Bi Dorothea Mabonye alisema benki hiyo Imekuwa ikishirikiana na taasisi za kijamii na mashirika yanayotoa huduma kwa wastaafu ikiwemo mifuko ya kijamii kama vile PSSSF na NSSF kutoa elimu ya kifedha kwa wanachama wao wanaotarajia kustaafu ndani ya muda mfupi ujao.

“Lengo letu ni kuongeza matumaini na furaha kwa wateja wetu hata pindi wanapostaafu. Tunataka kuhakikisha kwamba miaka ya baadaye ya wateja wastaafu wanakuwa na amani na furaha bila wasiwasi wa kifedha.’’ Aliongeza.

Habari Zifananazo

Back to top button