Serikali yaweka mikakati kuongeza thamani ya madini

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezwa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, ikiwemo kuimarisha sheria, kuongeza uwekezaji katika utafiti wa kina wa madini na kuandaa maeneo maalum ya uanzishwaji wa viwanda vya uchakataji.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali zake za madini kupitia shughuli za uchakataji, usafishaji na uyeyushaji wa madini ndani ya nchi badala ya kuuza nje yakiwa katika hali ghafi.

Akizungumza Novemba 21, 2026, wakati wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji (TMIC 2026), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Mavunde amesema Serikali imeweka msingi wa kisheria unaotaka madini kuongezwa thamani nchini kabla ya kusafirishwa nje.

Amesema Kifungu cha 133(1)-(5) cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kinaelekeza madini kuongezwa thamani nchini, huku kanuni zilizotungwa zikiainisha viwango vya uchakataji vinavyotakiwa kwa kila aina ya madini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha hakuna madini yanayotoka nchini bila kufanyiwa uchakataji unaotakiwa, hatua itakayoongeza manufaa ya kiuchumi na kuchochea ukuaji wa viwanda.

Katika kuhakikisha viwanda vinavyowekezwa nchini vinapata malighafi za kutosha, Mavunde amesema Serikali imeelekeza sehemu ya mapato yanayotokana na sekta ya madini, sawa na asilimia 10, kutengwa kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini.

Amesema hatua hiyo itaongeza wigo wa maeneo yanayofanyiwa utafiti na kutoa taarifa sahihi zitakazowasaidia wachimbaji, hususan wadogo, kuacha uchimbaji wa kubahatisha na kuongeza uzalishaji.

SOMA ZAIDI: Tanzania yatakiwa kutumia madini kujenga viwanda

Ameeleza kuwa Serikali pia inajiandaa kuanza utafiti mkubwa wa madini katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Lindi na Mtwara, ili kubaini rasilimali zilizopo na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vitakavyoanzishwa.

Aidha, amesema eneo la ekari 1,331 katika eneo la mgodi wa zamani wa Buzwagi, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, limetengwa na kubadilishwa kuwa Eneo Maalum la Kiuchumi la Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone) kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya madini.

Mavunde amesema Serikali pia inaendelea kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme, akieleza kuwa lengo ni kuongeza uwezo wa uzalishaji hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 ili kukidhi mahitaji ya viwanda vikubwa vya uchakataji na uyeyushaji wa madini.

Amesema hatua hizo zinalenga kuifanya sekta ya madini kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda, sambamba na kaulimbiu ya TMIC 2026 isemayo, ‘Madini Yaliyoongezwa Thamani: Kichocheo Kikuu cha Kukuza Uchumi na Maendeleo ya Viwanda’.

Kwa mujibu wa Mavunde, sekta ya madini kwa sasa inachangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku mchango wake katika uchumi ukiendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button