Waliofanyiwa uchunguzi  20% wana dalili za saratani

WATU 405 wamefanyiwa uchunguzi wa awali wa ugonjwa wa saratani kwa wananchi ambao hawaonyeshi dalili, ambapo kati ya hao waliofanyiwa uchunguzi wa awali asilimia 20 wamegundulika kuwa na dalili za awali za ugonjwa wa kansa ya matiti.

Mkurugenzi huduma za kinga kutoka hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, Dk.Crispin Kahesa, akizungumza wakati wa kambi hiyo mjini Kigoma alisema pamoja na kuwa hiyo mara ya kwanza kwa kambi hiyo kufanyika, huduma hizo za uchunguzi wa awali zimeanzishwa rasmi na zitakuwa zikifanyika kwenye hospitali ya Mkoa kigoma Maweni kila siku.

Dk.Crispin Kahesa Mkurugenzi Huduma za Kinga Hospitali ya Saratani Ocean Road. (Picha zote na Fadhil Abdallah).

Katika kambi hiyo ya uchunguzi ya awali ya upimaji wa saratani wanawake 172 walifanyiwa uchunguzi wa awali wa mlango wa kikazi, ambapo kati yao wanawake 13 wamegundulika kuwa na matatizo mbalimbali, huku watano wakiwa na dalili ya kansa ya mlango wa kizazi.

Advertisement

Amesema katika wanaume 66 waliojitokeza kupima tezi dume, kati yao wanaume 13 walikutwa na dalili za ugonjwa huo, hivyo taratibu zaidi za ushauri na matibabu zitaendelea kutolewa kwa watu hao.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na kuendesha kambi ya upimaji wa magonjwa, pia kambi hiyo imetumika kutoa mafunzo kwa watoa huduma wa hospitali hiyo, wakiwemo madaktari, manesi na wataalam wa vipimo, ili kuwawezesha kujua namna ya kushughulikia vipimo vya awali vya wagonjwa wa kansa.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za tiba katika hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni, Dk Frank Sudai alisema kuwa kambi hiyo ya upimaji wa magonjwa ya saratani imefanyika kwa mara ya kwanza, lakini imekuwa na mafanikio makubwa.

Dk.Frank Sudai Mratibu huduma za tiba Hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni

Dk.Sudai ambaye ni dakrati bingwa wa upasuaji, alisema kuwa zaidi ya watu 400 wamejitokeza na kufanyiw vipimo, ambapo ushauri umetolewa kwa ajili ya hatua zaidi kwa wagonjwa hao.

Alisema kuwa upimaji wa saratani haukuwa ukifanyika hospitalini hapo, lakini mafunzo yaliyotolewa kwa watoa huduma kutoka vitengo mbalimbali yatawezesha kuanza kufanya vipimo vya awali na wagonjwa watapewa rufaa kwa hatua zaidi za matibabu, tofauti na awali ambapo wagonjwa wote walikuwa wakianzia Hospitali ya Ocean Road.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *