Walioitwa NIDA wachangamke kuchukua vitambulisho visifutwe

JUZI Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilifanikiwa kutuma ujumbe mfupi wa simu (SMS) kwa wananchi 737,919 ambao hawajachukua vitambulisho vyao.

Iliwataka wananchi kwenda kuchukua vitambulisho vyao ofisi za Nida za wilaya katika maeneo yao.

Hatua hiyo inatokana na zaidi ya wananchi 200,000 kutochukua vitambulisho huku wananchi 520,000 wakiwa wamejitokeza kuchukua vitambulisho vyao.

Advertisement

Jambo la msingi ni kuhakikisha kila aliyetumiwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) anakwenda kuchukua vitambulisho na asipofanya hivyo, ukomo wa muda ukifika, namba za wahusika zinafutwa na mchakato utahitajika kuanza upya ili kupata kitambulisho hicho.

Vitambulisho hivi vinavyotolewa kwa mujibu wa Nida ni vilivyokaa muda mrefu katika ofisi za vijiji, mitaa, shehia na
kata bila kuchukuliwa na vinawahusu wananchi waliopata ujumbe wa simu tu.

Juzi Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji alisema mamlaka hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha vitambulisho
vyote vilivyotolewa vinachukuliwa na wahusika.

Mikakati hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyowapatia Nida Sh bilioni 42.5 za kununua malighafi na kuzalisha vitambulisho 13,738,735, hivyo kuondoa changamoto ya uhaba wa vitambulisho kwa wananchi wasionavyo.

Tunafahamu kwamba, tangu Septemba 2023, Nida ilianza uzalishaji na usambazaji mkubwa wa vitambulisho kupitia
ofisi za vijiji na mitaa, na hadi Desemba 2024, vitambulisho milioni 20.08 kati ya milioni 21.12 vilikuwa vimechukuliwa.

Hata hivyo, zaidi ya milioni moja bado vimebaki bila kuchukuliwa. Nida inasema sababu kuu za kutokuchukuliwa vitambulisho ni pamoja na wananchi kutegemea namba za utambulisho (NIN) pekee kupata huduma, kuhama kutoka waliposajili na baadhi ya wahusika kufariki dunia.

Sababu za kuhama na kifo hazikwepeki lakini hii sababu ya watu kuhudumiwa wakiwa na namba pekee ndio iliyofanya sasa kuwekwa ukomo wa namba hizo na ambao watachelewa kuchukua vitambulisho, vitafutwa.

Ni rai yetu kwa wananchi wenye namba na waliopokea ujumbe wa simu kuitikia mwito huu bila kusita ili kuhakikisha wanaendelea kupata huduma muhimu kwani bila kitambulisho hichi, wengi watakwama kupata huduma nyingi.

Nida imetoa fursa pia, kwa wananchi wenye vitambulisho vilivyofutika maandishi au sura kuvirejesha kwa ajili ya
kuchapishwa upya bila malipo na kwamba tayari vitambulisho 31,000 vilivyokuwa na changamoto hiyo vimechapishwa upya na vinaendelea kugawiwa.

Tunaipongeza Nida na TCRA kwa hatua hii na kuwahimiza wananchi kuitikia mwito huu na kuikumbusha Nida kuendelea kutoa vitambulisho kwa wananchi wote wenye sifa wanaopaswa kuwa navyo.