Waliorejesha ndege Dar waadhibiwa
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema imewachukulia hatua wote waliohusika na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za usafiri wa anga uliosababisha ndege ya Shirika la Ndege la Precision iliyokuwa inakwenda katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma kuamriwa irudi Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amelieleza HabariLEO kuwa Mei Mosi mwaka huu ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Precision namba PW 602 iliruka saa 12:11 jioni JNIA, Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Johari alisema ndege ilikuwa imebeba abiria 72 na kwa kawaida muda wa kuruka kufika Dodoma ni saa moja na kuwa ndege hiyo ilitarajiwa kutua kiwanja cha Dodoma saa 1:13 usiku muda ambao haukubaliki kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji uwanja wa Dodoma.
“Uchunguzi wa awali kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kurusha ndege kwani mwisho wa kutua unajulikana lakini bado ndege iliruhusiwa kuruka na ilitarajiwa kutua uwanja wa Dodoma saa 1:13 usiku, wakati taratibu zinaruhusu ndege mwisho kutoa saa 12:30 jioni,”alisema Johari.
Alisema baada ya taarifa hiyo, TCAA ilifanya uchunguzi zaidi na na imebaini kuwa taratibu na kanuni za usafiri wa anga zilikiukwa na hivyo wale wote waliohusika wamechukulia hatua.
“Uchunguzi umekamilika na tumebaini taratibu na kanuni za usafiri wa anga zilikiukwa na wote waliohusika tumewachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, tunaendelea kuwakumbusha ni lazima katika kutoa huduma kwenye sekta hii ya usafiri wa anga, taratibu, sheria na kanun izote zifuatwe, hatutamvumilia yeyote anayekiuka,tutamwajibisha,”alisema.
Akifafanua tukio hilo, Johari alisema kwa mujibu wa taratibu wa uendeshaji kiwanja hicho kimiundombinu (NOTAM) muda wa mwisho wa ndege kutua ni saa 12:30 jioni kwa sababu kiwanja hicho hakina taa za kuongozea ndege usiku.
“Hiyo ni kwa sababu miundombinu ya uwanja huo ambayo imebainishwa katika waraka NOTAM namba B 0027/23, B 0026/23, B0025/23, B0024/23 na B0023/23.
Uwanja wa Ndege wa Dodoma unaendeshwa kwa kuangalia mawio na machweo ya jua. Na hiyo ni kulingana na taarifa za usalama wa anga namba GEN 2.7-4 ya Januari 5, mwaka 2017,”alisema Johari.
Hata hivyo alisema pamoja na kuwepo kwa taratibu na kanuni hizo ambazo zinafahamika, ilipofika saa 12:48 jioni rubani wa ndege hiyo namba PW 602 alishauriwa na mwongoza ndege aliyeko kwenye mnara wa kuongozea ndege kutotua Dodoma na badala yake ageuze ndege kurudi uwanja wa JNIA .