MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Shinyanga imewapongeza na kuwapa zawadi baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wazalendo na waaminifu kwa kulipa kodi vizuri kwa hiyari.
Pongezi hizo zimetolewa leo Desemba 19, 2024 na Mwanasheria wa TRA kutoka Makao Makuu, Elisha Shigela kwa niaba ya Kamishna wa Mamlaka hiyo, Yusuph Mwenda ambapo amesema baadhi ya wafanyabiashara wamejua kazi yao.
Shigela amesema wameamua kutoa zawadi ili wafanyabiashara wakuwe na waendelee na biashara zao kuisaidia serikali na hawapo kwaajili ya kuua biashara.
“Mjenga nchi ni mwananchi hivyo wafanyabiashara baadhi wametekeleza kazi yao na serikali imethamini michango yao,” amesema Shigela.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Gilitu Enterprises Manispaa ya Shinyanga, Gilitu Makula amesema wameipongeza serikali kwa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mafuta ya kupikia kwani ni eneo ambalo lilikuwa likiwapa changamoto na sasa wanalipa kodi vizuri kwa maendeleo ya nchi..
“Ninawapongeza sana TRA kufikisha kilio chetu kwa Rais kwani zamani nilivyokuwa naaza uzalishaji changamoto ya ulipaji kodi ilikuwepo lakini sasa nalipa vizuri nakujua umuhimu wake napongeza sana kuthamini mchango wangu,”amesema Makula.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment iliyopo Manispaa ya Shinyanga Gasper Kileo ameishukuru TRA kwa kujua mchango wake na kuwa mzalendo wa ulipaji kodi vizuri.
Mfanyabiashara kutoka Manispaa ya Shinyanga Clesensia Ernest amesema wanalipa kodi kwa kutambua umuhimu wake kwani fedha hizo ndizo zinazojenga miundombinu ya barabara, afya, maji na umeme.