WAMILIKI wa migodi na wafanyabiashara wa madini ya vito Spinel katika kijiji cha Ipango kilichopo mji wa Mahenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro wameiomba serikali kupeleka huduma ya mawasiliano ya simu kurahisha shughuli za uchimbaji madini.
Huduma ya upatikanaji wa mawasiliano na nishati ya umeme wa uhakika katika migodi ya spinel inaweza kusaidia shughuli za uchimbaji na wamiliki wa migodi wanaweza kuzalisha zaidi bila kuingia hasara kubwa kama ilivyo sasa.
Akizungumza wa waandishi wa habari wakati wa ziara ya mgodi wa Franone Mining and Gems wanaozalisha madini ya Spinel kwa lengo lakupata elimu kuhusu madini hayo, Meneja Mgodi Elias Thomas amesema wamekuwa na changamoto ya mtandao wa simu za mkononi ambapo mtandao unaopatikana ni mmoja tu ambao pia unapatikana kwa shida.
Thomas amesema huduma ya mawasiliano ya simu za kiganjani ni muhimu hususani maeneo ya migodini kutokana asili ya kazi zao hivyo ni muhimu kwa serikali kulipatia kipaumbele suala hilo.
Aidha Thomas amesema kupitia uzalishaji wa madini ya Spinel wameweza kurudisha kile wanachokipata kwa jamii kwa kujenga nyumba sita kwa wananchi waliokuwa na uhitaji ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara na kujenga vyumba vya madarasa.
Akizungumzia kuhusu kukatika kwa umeme hasa katika maeneo ya migodi amesema hali hiyo inachangia kuendesha uzalishaji kwa hasara hata serikali pia kukosa mapato ambapo amaiomba serikali kuhakikisha maeneo yote ya migodi yanakuwa na umeme wa uhakika.
“Mgodi umetoa ajira kwa vijana zaidi ya 200 ambao ni wazawa na pia tumekuwa tumechangia uchumi wa nchi kwa kuwa waaminifu katika ulipaji wa kodi na tunaahidi serikali kuendelea kulipa kodi kwa uaminifu pia kuchangia maendeleo ya maeneo yanayotuzunguka ambapo tunachimba madini. “amesema Thomas.
Kwa upande wake Semeni Bakari ambaye ni mama lishe katika mgodi huo ameipongeza ambapo amesema uwepo wa mgodi umesaidia kuwepo kwa miundo mbinu mizuri hasa upande wa barabara ambapo kwa sasa zinapitika muda wote.
Amesema anamshukuru pia mwekezaji mzawa Onesmo Mbise maarufu kwa jina la Onee kwa kuwekeza katika eneo hilo kwa kuwa wameweza kujipatia ajira na wanaendesha maisha yao bila shaka yoyote na wanaendelea kuimarika kiuchumi.
Jesse Mtui ambae ni mfanyakazi wa mgodi huo amesema kupitia mgodi huo ameweza kupata ajira ambayo inamsaidia katika kuendesha maisha yake na kujijenga kiuchumi tofauti na awali.
Ameongeza kuwa kukosekana mawasiliano ya simu za kiganjani yeye kama kijana inampa wakati mgumu kwa kuwa yuko mbali na familia yake hivyo anakosa kuwasiliana nao kwa wakati.