Wamuomba Mbowe agombee uwenyekiti taifa

WENYEVITI zaidi ya 20 wa mikoa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) waliojitokeza hadharani kumuomba na kumshawishi mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe achukue fomu ya kutetea tena nafasi yake hiyo.

Viongozi hao kutoka mikoa mbalimbali walijitokeza nyumbani kwa Mbowe, Mikocheni Dar es Salaam wakisema watamuunga mkono katika uchaguzi wa kitaifa wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwakani Januari.

Katika mazungumzo yake wakati wakimuomba Mbowe, wamesema miongoni mwa hoja walizozitaka za kumtaka mwenyekiti wao huyo agombee kwa mara nyongine ni pamoja na ubunifu.

Advertisement

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, William Mungai amesema kutokana na ubunifu wa Mbowe ndiyo maana Chadema imeandelea kuwa imara kwa miaka mingi.

Amesema mkongwe huyo wa siasa amebuni oparesheni mbalimbali ambazo zimewezesha chama kupata wanachama zikiwemo oparesheni Sangara na Movement for Change na kwamba hawana uhakika na wagombea wengine iwapo watasaidia katika kuongeza wanachama.

Katika hoja hiyo ya ubunifu pia amesema kwamba ni Mbowe amebuni nguo, bendera na alama nyingine za chama ambazo zimepata umaarufu na zinatumika mpaka leo.

Amesema Mbowe ana uwezo wa kujenga viongozi ambao wengine wamechukuliwa na vyama vingine na kuwa viongozi katika vyama hivyo na wengine kupata uongozi serikalini ikiwemo baadhi kuwa wakuu wa Wilaya, wakuu wa mikoa na hata mawaziri.

Amesema Mbowe ni ‘States Man’ na jasiri wa vita asiyeogopa mapambano na sio mtu wa matamko tu kama wengine akitolea mfano alivyoweza kujitokeza katika maandamano waliyoyatangaza Mwezi ambapo alijitokeza akiwa na binti yake.

“Chini ya uenyekiti wako unapokuwa na jambo huwa tunaona una mipango na unajua tunaendaje” alisema Mungai.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Ally Kadogoo alisifu uongozi wa Mbowe kuwa ni wa kutoa fursa sawa kwa watu wote akijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba alipotoka hakuwahi kuwa hata mjumbe wa mtaa lakini kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani.

Ametupa vijembe kwa wagombea wengine kwamba wamezoea ‘kuropoka’ mambo ya ndani ya chama na kwamba hawafai kuwa viongozi.