DAR ES SALAAM: VIONGOZI wa Baraza la Madiwani, viongozi wa kiislamu na watoto yatima wamekutana kumuombea dua Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kutoa zaidi ya Sh bilioni 317 zilizotumika kuboresha miradi ya maendeleo jijini Dar es Salaam.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto ameeleza hayo katika hafla fupi ya Iftar iliyoandaliwa na Ofisi ya Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyofanyika jana katika viwanja vya Karimjee.
Mufti Mkuu wa Tanzania, Dk Abubakary Zubeir ametoa shukrani kwa uongozi huo kwa kuandaa hafla hiyo, ambapo amesema kuwa imekuwa fursa muhimu kuwaunganisha Waislamu na wasiokuwa Waislamu.
SOMA ZAIDI: RC Mtwara ataka dua zaidi uchaguzi mkuu 2025
Aidha, ametumia muda huo kuwakumbusha waumini wa dini ya Kiislamu kuutumia mwezi wa Ramadhani kama kipindi cha kujifunza na kutenda mambo mema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, kumefanyika maendeleo makubwa, hususan katika Mkoa wa Dar es Salaam. Amesema kuwa hafla hiyo ilikuwa pia ni nafasi ya kumshukuru Mungu kwa uongozi wa Rais Samia na kumuombea dua na mafanikio katika utendaji wake.