SHIRIKISHO la Mchezo wa Bao Tanzania (Shimbata) limemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia gharama za matibabu Rais wa shirikisho hilo Monday Likwepa aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo (JKCI) Muhimbili akisumbuliwa na moyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam leo Mmoja wa wajumbe wa Shimbata Sheikh Rashid Kayumbo amesema Likwepa alilazwa kwenye taasisi hiyo tangu Jumanne ya wiki hii na mpaka sasa gharama za matibabu zinazohitajika ni sh milioni 20.
Amesema Likwepa alianza kusumbuliwa na tatizo hilo mara baada ya kurejea kutoka Kazakstan kwenye mashindano ya kimataifa ya mchezo wa bao Oktoba mwaka huu.
“Sisi kama Shimbata tunamuomba Rais Samia akubali kumsaidia gharama za matatiba Monday Likwepa kwa kadiri inavyostahili kwani ni kiongozi ambaye alibeba maono ya Mwalimu Julius Nyerere kuhakikisha mchezo huo unafanikiwa nchini,”alisema.
Kwa mujibu wa Kayumbo, Likwepa anastahili kusaidiwa kwa kuwa ndiye Mtanzania pekee aliyekwenda Kazakstani bila udhamini wa taasisi wala kampuni yoyote kuwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Likwepa pia, aliuenzi mchezo huo ambao ulikuwa ukipendwa na viongozi mbalimbali na hasa Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Nyerere kiasi cha kuutambulisha kwa viongozi wakubwa duniani.
Itakumbukwa Nyerere alibeba bao na kusafiri nalo mpaka Ikulu ya Marekani kwenda kumfundisha Rais John Kenedy mwaka 1963 na mwaka 1965 alisafiri tena na bao hadi China kwa Rais Mao Zedong. Pia, aliwahi kuutambulisha kwa Rais wa Ghana Nkwame Nkuruma na Patrice Lumumba wa DRC.
Mjumbe huo amesema ikimpendeza Rais Samia ampe tuzo Likwepa na shirikisho hilo na wote waliosapoti mchezo huo kwa kuendelea kuuenzi mchezo huo na kuzungumzia umuhimu wa kuwasapoti wakati wote ili kuufikisha kwenye maono yaliyokusudiwa.