Wanafunzi Bunda wapewa elimu ya kujitambua

WANAFUNZI 1,298 wa shule za sekondari Kunzugu, Sizaki na Paul Jones zilizopo wilayani Bunda mkoani Mara wamejengewa uwezo kwa kupewa elimu ya kujiamini na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike na kiume.

Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Grumeti Fund kupitia idara ya maendeleo ya jamii.

Advertisement

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo katika sekondari ya Kunzungu, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Grumeti Fund, Frida Mollel amesema lengo la kongamano hilo ni kuwaelimisha vijana wa kike na kiume kutambua thamani yao sambamba na kuwajengea uwezo wa kujiamini na kufikia ndoto zao huku akiwataka kumtanguliza Mungu katika kila jambo kwani ndio msingi wa mafanikio.

“Vijana wengi sasa wametumbukia katika tabia hatarishi ambazo kupitia tabia hizo ni ngumu kufikia ndoto zenu, ili muweze kufikia ndoto zenu na kuwa vijana wakutegemewa katika familia na taifa kwa ujumla,” amesema.

Aidha Frida amewataka vijana hao kujiepusha na matumizi ya mitandao ya kijamii kabla ya wakati lakini pia hata watakapoanza kuitumia mitandao hiyo waitumie kwa manufaa na sio vinginevyo.

Katika hatua nyingine,mkufunzi kutoka chuo cha Afya Kisare, Restuda Murutta amewaasa wanafunzi wa kike kuzingatia usafi wawapo katika siku za hedhi ambapo amewashauri  wanafunzi hao  kuzitumia taulo za kike zilizotolewa na Grumeti Fund.