Wanafunzi Bwiru, Buswelu waripoti shuleni
WANAFUNZI 441 wameripoti katika shule za sekondari Bwiru wasichana, Bwiru wavulana na Buswelu zilizopo katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. Masomo ya kidato cha tano yanatarajia Jumatatu ya Agosti 21,2023.
Akizungumza leo na HabariLEO, katika shule ya sekondari ya wasichana ya Bwiru, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Mariam Msengi amesema kwa wilaya yao wanatarajia wanafunzi 745 kujiunga na kidato cha tano lakini mpaka leo ni wanafunzi 441 wameripoti.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Bwiru Mecktilda Shija amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuweza kuleta Sh milioni 215 kwajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya Bweni moja, matundu matano ya vyoo na madarasa matatu.
Amesema katika shule yao wanatarajia kupokea wanafunzi 509 wa kidato cha tano lakini mpaka sasa ni wanafunzi 205 wamesharipoti.
Amesema bweni waliojengewa na Serikali lina uwezo kubeba wanafunzi 80 na kuna vyumba 10 na kila chumba kina uwezo wa kubeba vitanda viwili.
Amesema uongozi wa shule yao umefanikiwa kununua vitanda na kila mwanafunzi analala katika kitanda chake.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Kiomoni Kibamba amesema Juni 30 mwaka huu walipokea fedha Sh milioni 381 kwajili ya kujenga shule mpya ya sekondari Kiseke.
Amesema mpaka sasa tayari manispaa yao wamepokea Sh milioni 60 kwajili ya kujenga madarasa mawili mapya katika shule ya sekondari ya wasichana Bwiru.
Amemshukuru mkuu wa mkoa wa Mwanza Amos Makalla kwa usimamizi mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Ilemela.