Wanafunzi Dar wapewa elimu ya fedha

DAR ES SALAAM: Shirika la Hazina SACCOS limetoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga kizazi chenye nidhamu ya kifedha na uwezo wa kujitegemea.

Mafunzo hayo yalienda sambamba na mashindano ya elimu ya fedha kwa wanafunzi, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha, utunzaji wa akiba na uwekezaji mdogo mdogo tangu wakiwa mashuleni.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Hazina SACCOS, Dk. Festo Mwaipaya, alisema lengo la shirika hilo ni kujenga jamii yenye uelewa mpana wa masuala ya fedha, mtazamo chanya kuhusu uchumi binafsi na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

Alisisitiza kuwa elimu ya fedha inapaswa kuanza kutolewa mapema ili kuwasaidia vijana kuwa na misingi imara ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Angela Nalimi, alisema kupitia vilabu vya Hazina SACCOS vilivyoanzishwa mashuleni, wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza misingi ya matumizi sahihi ya fedha, utamaduni wa kuweka akiba, pamoja na misingi ya kukopa na kurejesha mikopo kwa uwajibikaji.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inachangia kukuza vipaji vya ujasiriamali miongoni mwa vijana.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo walieleza kunufaika kwa kiasi kikubwa, wakisema wamepata uelewa kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, kupanga matumizi yao ya kila siku na kujiandaa na maisha ya baadaye kwa misingi bora ya kifedha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button