WANAFUNZI 1643 wa Shule ya Sekondari Msalala iliyopo Halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita wameongezewa hamasa ya ufaulu kwa kujengewa bweni na bwalo lenye zaidi ya sh bilioni moja na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu.
Pia Mgodi huo kupitia fedha za huduma kwa jamii (CSR) kwa bajeti ya mwaka 2022/2023 ulitenga Sh milioni 50 kwaajili ya mpango wa kuongeza ufaulu (PIP) kwa kutoa chakula kwa wanafunzi wa kidato cha nne na kuwapatia motisha walimu watakao faulisha masomo yao.
Hayo yamesemwa na Mrakibu Idara ya Mahusiano kutoka mgodi huo, William Chungu baada ya kutembelea ujenzi wa bwalo na bweni na kujionea hali ya ufaulu hasa kwa wanafunzi wa kike ambao walikuwa hawafanyi vizuri kipindi cha nyuma katika mitihani ya taifa.
Kaimu mkuu wa shule hiyo, John Marry Stephen alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1996 kwa sasa kuna wanafunzi 1643 ambapo wa kike ni 990 na wakiume 653 kwenye historia kipindi cha nyuma wanafunzi wa kike walikuwa hawafanyi vizuri.
“Kuwepo kwa bweni la wasichana kumesaidia ufaulu wanafunzi zaidi ya kumi wamechaguliwa kuingia kidato cha tano na kidato cha pili kupata daraja A wengi kwa mwaka jana zamani walikuwa wavulana pekee na walimu wanajitahidi kufundisha na kufanya vizuri ili kupata motisha ”alisema Mwalimu Stephen.
Mwalimu Stephen alisema wanafunzi wa kike walikuwa wakiacha shule sababu ya kutembea umbali mrefu nakukutana na vishawishi njiani lakini sasa bweni lipo kwa wanafunzi wa kike pekee imesadia idadi kubwa kumaliza shule.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne, Leonard Daniel na Tusajigwe George walisema bweni limesadia wao kupata muda wa kujisomea kwa pamoja pia walikuwa wakishindwa kufika shule kwa kupata vitisho vya fisi njiani nakurubuniwa na madereva wa bodaboda.
Ofisa mipango wa halmashauri hiyo, Angela Kiwia alisema vijiji viwili vinavyozunguka mgodi huo ndiyo vinanufaika na mapngo wa kuongeza ufaulu umesadia hamasa kwa walimu na wanafunzi na Sh milioni 50 zinazotolewa zinajumuisha chakula kwa wanafunzi wa kidato cha nne pekee wazazi hawachangii chochote.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Husna Toni alisema kuanzia mwaka 2018 hadi 2023 wamepokea zaidi ya Sh bilioni 4.4 kutoka kampuni ya Barrick Bulyanhulu kwaajili ya sekta ya maendeleo ikiwemo elimu.