Wanafunzi Muhas, Ufaransa kubadilishana ujuzi afya

DAR ES SALAAM: UFARANSA kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili ( MUHAS ) wanaendelea kuboresha uhusiano wao ambapo sasa wanafunzi wa chuoni hapo watapata nafasi kwenda nchini humo kujifunza masuala mbalimbali ya afya.
Sambamba na hilo, walimu na wanafunzi kutoka Ufaransa pia watapata nafasi ya kuja Muhas kufundisha na kujifunza katika maeneo tofauti ya afya.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Ave
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne Sophie Avé amesema Ufaransa ina mengi ya kujifunza kutoka Tanzania katika afya kwani yapo magonjwa ambayo taifa hilo hawayafahamu.
“Kwa mfano, unajua hatuna wagonjwa wengi na wakati mwingine tunapokuwa na kesi za malaria hatuwezi kutambua kwa sababu hatuna,” alisema Balozi huyo.

Alisema kuna mkataba wa maelewano kati ya chuo na Chuo Kikuu cha Bordeaux cha dawa ambapo pia kinatoa masomo ya kijamii kuhusu afya, hivyo vitashirikiana katika mafunzo mbalimbali.
Aidha, alieleza kuwa fursa ya ushirikiano pia inalenga kubadilisha ujuzi, uwezo na kudumisha ushirikiano wao hasa kwa vijana ambao ndio nguzo ya maendeleo kwa baadaye.

Makamu Mkuu wa Muhas anayeshughulikia taaluma, Profesa Emmanuel Balandya alisema chuo hicho kina uhusiano mzuri na Urafansa katika maeneo ya tafiti, tiba na elimu.

Makamu Mkuu wa Muhas anayeshughulikia taaluma, Profesa Emmanuel Balandya
Alisema ushirikiano huo unalenga mwendelezo mzuri katika eneo la afya ambapo fursa ya wanafunzi Muhas kupata mafunzo Urafansa itaongeza wigo mpana kuongeza wataalamu wa afya nchini.



