Wanahabari Mtwara wakumbushwa maadili uchanguzi

MTWARA: KUELEKEA Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, waandishi wa habari mkoani Mtwara wametakiwa kuandika na kuripoti habari kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Rai hiyo imetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Malima Zacharia ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Year Book wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani humo.
Mafunzo hayo ni ya siku moja yaliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani yenye lengo la kuwajengea uwezo waandishi hao kuhusu namna bora ya kuripoti habari za uchaguzi kwa kutenda haki na kufuata misingi ya taaluma na bila kupendelea upande wowote.

Amesema wajibu wa vyombo vya habari ikiwemo kusimamia maslahi ya umma wakati wa uchaguzi, amani na usalama wa wananchi pia amezungumzia suala la mtazamo wa kitaaluma kwa vyombo hivyo kuwa ni mwangalizi wa uwazi na mwalimu wa umma.
Hata hivyo amewataka waandishi hao kuwa mchango wakati wa mchakato huo wa uchaguzi kwa kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi lakini pia kuepuka kuchochea, kushirikisha wagombea na kuripoti kampeni.

Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) Bryson Mshana amesema ipo changamoto kubwa kwa baadhi ya waandishi kuandika habari kwa kuangalia maslahi yao binafsi bila kuangalia maslahi ya taifa.
“Tuna changamoto kubwa ya waandishi wa habari na vyombo vya habari kuandika habari kwa kuangalia hatima yao wenyewe na sio hatima ya taifa, waandishi waandika kwa ajili ya kupata nafasi za uteuzi hili jambo ni baya sio zuri kwasababu linaweza kufikisha nchi mahali pabaya,”amesema Mshana.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Sheda Masha ameshukuru kwa kupata mafunzo hayo ambayo yanalenga kuwakumbusha wajibu wao katika kutekeleza majukumu hayo na kuahidi kufanyia kazi katika uchaguzi mkuu huo.
Mafunzo hayo yameendeshwa na Shule Kuu ya Uwandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


