Wanahabari watakiwa kujitafakari

DAR ES SALAAM: WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kujitafakari na kuzingatia taarifa wanazotoa kwa ummana kuongoza ajenda za msingi hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi ambazo zitasaidia kupatikana kwa uchaguzi huru na wa haki.
Wito huo umetolewa na Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, katika mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na mtandao huo, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yalihusisha waandishi wa habari zaidi ya 130 kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Wakili Olengurumwa amesema kuwa waandishi wa habari wana jukumu kubwa katika kipindi hiki cha uchaguzi, hivyo ni muhimu wakazingatia maadili, sheria na kanuni zinazowaongoza, ili kutoa taarifa sahihi na zenye kujenga jamii.
“Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu sheria za uchaguzi, usalama na ulinzi wao, pamoja na umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma yao wakati wa uchaguzi,” amesema Olengurumwa.
Aidha, amewaomba viongozi wa kitaifa akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, vyama vyote vya siasa pamoja na taasisi za uchaguzi kutambua umuhimu wa kuwa na majadiliano ya kitaifa ili kufikia mwafaka. Ambapo amesema kuwa THRDC wako tayari kusaidia mchakato huo endapo pande zote zitaridhia kukaa meza moja kujadili malalamiko na changamoto zinazowakabili ili zifanyiwe kazi.
“Natoa wito kwa Mheshimiwa Rais, vyama vya siasa pamoja na taasisi za uchaguzi kuona umuhimu wa kuwa na majadiliano ya kitaifa. THRDC tupo tayari kusaidia kama pande zote zitakubali kushiriki. Lengo ni kuhakikisha tunafika Oktoba kama taifa moja lenye maridhiano,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Habari Tanzania, Kenneth Sibaya, amewataka waandishi wa habari kuwa wavumilivu licha ya changamoto wanazokumbana nazo, na kuendelea kufanya kazi kwa moyo wa kujitolea kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.
“Waandishi wa habari mnapaswa kufanya kazi hii kwa moyo wa dhati, bila kujali maslahi binafsi, ili kusaidia jamii na kuhakikisha kazi yenu inaonekana kuwa ya baraka na si ya laana,” amesema Sibaya.
Naye mwandishi mkongwe, Deus Kibamba, amezungumzia kuhusu changamoto ya mifumo ya uchaguzi barani Afrika, aambapo ameeleza kuwa ni mibovu na yenye changamoto nyingi. Amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kufuatilia mifumo hiyo, kutambua chanzo cha matatizo na kupendekeza njia za kuleta mabadiliko yatakayowezesha uchaguzi huru na wa haki.
Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa zoezi la kugawa makoti maalum kwa waandishi wa habari kwa ajili ya utambulisho na usalama wao pindi wanapotekeleza majukumu yao, pamoja na ugawaji wa vyeti kwa washiriki waliokamilisha mafunzo hayo.



