Wananchi DRC tulieni mahakama itende haki

DESEMBA 20, mwaka uliopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo ni moja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ilifanya uchaguzi mkuu ambao pamoja na viongozi wengine, ulikuwa kumchagua rais.

Awali, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) ilitangaza watia nia 26 waliokidhi vigezo vya kugombea kiti cha urais akiwamo Felix Tshisekedi aliyejitosa kuwania kiti hicho kwa muhula wa pili wa miaka mitano. Kabla ya uchaguzi huo na hata sasa, Tshisekedi ndiye Rais wa DRC.

Hata hivyo, baadaye wagombea wanne walijiondoa na kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani hivyo kinyang’anyiro kikabaki kwa wagombea 22.

Desemba 31, 2023, CENI ilitangaza matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais ikibainisha kuwa, Rais Tshisekedi ameshinda kwa takribani asilimia  73 ya kura, huku mpinzani wake wa karibu, Moise Katumbi, akipata asilimia 18 ya kura zilizopigwa.

Mgombea mwingine aliyekuwa na ushindani mkubwa ni Martin Fayulu ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo kwa kupata takribani asilimia tano ya kura zilizopigwa.

Mbali na wagombea hao watatu, hakuna mgombea mwingine kati ya waliosalia aliyepata zaidi ya asilimia moja ya kura zilizopigwa.

Mwenyekiti wa CENI, Denis Kadima, alikiri kuwepo kwa dosari kadhaa zilizoshughulikiwa vizuri na akasisitiza kuwa, matokeo hayo yanaakisi matakwa ya watu wa DRC.

Kadima alisema wagombea kadhaa wa upinzani wanataka uchaguzi mpya kwa sababu wanajua walishindwa.

Rais mteule amepangwa kuapishwa Januari 20 baada ya Mahakama ya Kikatiba ya DRC kuidhinisha matokeo hayo ya uchaguzi, Januari 10, mwaka huu.

Tunawapongeza wananchi wa DRC kwa ukomavu wa kufanya uchaguzi na kupokea matokeo katika hali ya usalama.

Huo ni ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia unaotambua na kuzingatia kuwa, uchaguzi ni kwa ajili ya watu na si watu kwa ajili ya uchaguzi.

Ni ukomavu kwa wanasiasa na wadau wote wa uchaguzi huo wanaokubali ukweli kuwa, ‘asiyekubali kushindwa si mshindani’.

Sasa, baada ya uchaguzi na matokeo kutangazwa, wananchi waviachie vyombo husika ikiwamo Mahakama ya Katiba kutimiza wajibu wake wa kutoa haki kwa pande zote, badala ya kutumia nguvu na muda mwingine kwa ‘ubishi.’

Kwa kuzingatia umuhimu wa uchaguzi wa kidemokrasia, umuhimu wa amani na usalama sambamba na umuhimu wa rasilimali muda na watu, tunawahimiza wananchi wa DRC watulie na kusubiri mahakama itekeleze wajibu wake ili kama itathibitisha matokeo yaliyotangazwa na CENI kesho Januari 10, basi imwidhinishe mshindi wa urais, Tshisekedi ili aapishwe Januari 20, 2024 na kazi ya kuijenga DRC iendelee maana kuna maisha baada ya uchaguzi.

Ni kutokana na ukomavu na utulivu uliotawala katika kipindi cha kusubiri kutangazwa kwa mshindi, tunasema wananchi DRC tulieni mahakama itende haki.

Habari Zifananazo

Back to top button