Wananchi Kitaya washukuru ujenzi wa barabara

WAKAZI wa kijiji cha dindwa kata ya kitaya Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara wameiskuhuru serikali kwa kuwaletea mradi wa barabara ya Kitaya, Mbembaleo Nanyamba ya kilometa 2.4 inayogharimu zaidi ya Sh bilioni 1.
Hayo yamejiri wakati Mbubge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota alipotembelea kwenye jimbo hilo kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo ikiwemo ya barabara, elimu pamoja na maji.

Mkazi wa kijiji cha dindwa kwenye kata hiyo, Salum Mohamed amesema kabla ya mradi wakazi hao walikuwa na changamoto kubwa ya barabara kwani gari zilikuwa hazipiti na badala yake walikuwa wakitumia usafiri wa baiskeli au pikipiki.
“Hadi kufikia hatua hii ya sasa tunaishukuru serikali yetu kwasababu tumeondokana na changamoto iliyokuwa inatukabili kwa muda mrefu, sasa tunapata urahisi wa kwenda mjini”amesema Salum
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo usafirishaji wa mazao kama vile korosho pia kutachochea maendeleo ya wakazi wa maeneo hayo.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mtwara, Mhandisi Elisha Ndadila amesema mradi huo ni wa miezi nane ambao ulianza Agosti 2024 na unatarajiwa kumalizika Aprili 2025.
Mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 25 ya utekelezaji huku malengo yalikuwa ufikie asilimia 75 ya utekelezaji mpaka sasa ambapo uko chini ya Mkandarasi Serc Construction Company Ltd.
Mbunge wa Jimbo hilo, ameusisitiza uongozi wa halmashauri hiyo kuendelea kusimamia mradi ili uweze kukamilika kwa wakati wananchi wapate huduma.
“Tuuone kama mradi huu ni wa kwetu tuendelee kuusimamia kwa ukaribu zaidi ili ukamilike Kwa wakati wananchi waweze kunufaika na mradi”amesisitiza Chikota


