Wananchi Monduli waisifu CCM ‘Kadogoo’ kurejeshwa

ARUSHA: WANANCHI wa Jimbo la Monduli mkoani Arusha wameishukuru Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa uamuzi wa kurejesha jina la Isack Joseph Copriano maarufu kwa jina la “Kadogoo” kuwa mgombea ubunge kupitia chama hicho.
Katika hafla ya kuchukua fomu za kugombea ubunge, wananchi mbalimbali walieleza furaha yao na kusema uamuzi huo umeonesha CCM kusikiliza sauti ya wananchi na kuweka mbele maslahi ya Jimbo hilo.
Frank Mwaisumbe, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli na Longido amesema Kamati Kuu imefanya uamuzi sahihi bila kuangalia umaarufu bali uwezo wa kiongozi.
“Kadogoo ni mtoto wa mkulima na mtendaji anayeshughulika na shida za wananchi. Ninamfahamu kwa ukaribu wake na utendaji wake wa kazi,” amesema Mwaisumbe.
Naye Siomi Laizer, mkazi wa kijiji cha Naalarami, amesema wananchi wa Monduli wako tayari kumpa ushirikiano Copriano ili kuhakikisha ushindi wa CCM na kuendeleza maendeleo ya Jimbo hilo.
Lebiruka Komite, mkazi wa Monduli, alisema wananchi wanamchukulia Copriano kama kiongozi wa vitendo na si maneno, jambo linalowapa imani kubwa kuelekea uchaguzi.

Kwa upande wake, Namnyaki Julius Mollel amesema kurejeshwa kwa jina la Copriano ni kama majibu ya maombi ya wananchi.
“Mungu amesikia kilio chetu kwa sababu Kadogoo amewafanyia mambo mengi, ikiwemo kushughulikia migogoro ya mipaka ambayo ilitutesa kwa muda mrefu,” amesema Mollel.
SOMA ZAIDI
Vyombo vya habari vyatakiwa kufuata sheria,kanuni za uchaguzi
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Copriano alisema ameupokea uteuzi huo kwa moyo mkunjufu na ataendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha kura za ubunge na za Rais zinapatikana kwa wingi Jimboni humo.
“Nitajitahidi kwa hali na mali kuhakikisha kura za chama chetu zinatosha, lakini zaidi nitakuwa karibu na wananchi kusikiliza na kushughulikia changamoto zao,” amesema Copriano.
Kwa upande wake, Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Monduli, Emmanuel Mpongo, alisema maandalizi yanaendelea vizuri na aliwataka wagombea wote kuendesha kampeni kwa amani na kuzingatia kanuni na sheria.


