Wananchi Mtwara kupewa elimu kupinga rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU ) mkoani Mtwara imeandaa mkakati maalum wa kuwaelimisha wananchi kuhusu vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akizungumza leo Novemba 6, 2024 mkoani hapa, Naibu Mkuu wa Takukuru, Jumbe Makoba amesema watumishi wa taasisi hiyo watafuata wananchi sehemu za mikusanyiko ikiwemo kanisani na misikiti ili kuwaelimisha
‘Lengo la mkakati huo ni kuelimisha jamii kukataa rushwa hasa kwenye suala la uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu,” amesema.
Akizungumza katika ibada ya jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki, Makoba aliwataka waumini kuomba ili kuwepo na uchaguzi wa haki ambao utapelekea kuwapata viongozi watenda haki ya kuliongoza taifa kwa haki.
Amesema wanaomba uongozi wakitumia rushwa husababisha ukosefu wa haki kwa wananchi na taifa wanaowaongoza.
Akinukuu maandiko katika kitabu cha Hosea 8:3-4, Makoba amesema taifa likisimamisha viongozi ambao wanatoa rushwa litakuwa limejitengenezea viongozi ambao ni sanamu.
‘Ukisoma katika maandiko matakatifu unaona kwamba viongozi au wafalme waliongoza pasipo shauri la Mungu yaani wala rushwa ni kama sanamu, zina vinywa lakin hazisemi, zina macho lakini hazioni..,’ amesema na kuwataka waumini kuomba kwa bidii ili kuwezesha Tanzania kupata viongozi walio na maadili na hofu ya Mungu.



