Wananchi Namtumbuka waomba kuongezewa walimu

WAKAZI wa kijiji cha Namtumbuka shuleni kata ya namtumbuka Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara wameiomba serikali kuwaongezea walimu katika shule ya msingi namtumbuka kutokana na uwingi wa wanafunzi shuleni hapo.
Hayo yamejiri wakati Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota alipotembelea katani hapo na kupata fursa ya kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliyofanyika kijijini hapo.
Azungumza wakati wa mkutano huo wa hadhara, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Namtumbuka, Jafari Matendo amesema shule hiyo ina walimu 4 huku idadi ya wanafunzi ikiwa ni 556 ambapo kutokana na idadi hiyo kubwa ya wanafunzi ipo haja kwa serikali kuongeza walimu shuleni hapo.
“Tunaiomba serikali ituangalie swala hili la walimu kwasababu watoto ni wengi walimu wachache lakini pia swala la kutuboreshea miundombinu ya madarasa kwasababu hii shule ni ya mda mrefu”amesema Matendo
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mtwara Vijijini, Nashir Mfaume amesema kitendo cha mbunge huyo kutembelea katika kata zao ikiwa ni pamoja na kusikikiza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao katika maeneo yao ikiwemo hiyo ya elimu lakini kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hata hivyo ni fursa kwa wananchi hao kupata fursa ya kuleta kero zao mbele ya mbunge huyo ili mwisho wa siku ziweze kufanyiwa kazi.
Nae mbunge wa jimbo hilo kuhusu changamoto hiyo ya shule amekiri kuwa ni kweli walimu hao 4 waliyopo kwa sasa hawatoshi kulingana na uwingi wa wanafunzi hao.
Hata hivyo kuna mchakato unaendelea wa kupata walimu kwenye halmashauri hiyo na shule hiyo ni miongoni mwa shule itayoletewa walimu pamoja na kufanyiwa maboresho na mahitaji ya walimu shuleni hapo ni 12 huku upungufu ukiwa ni walimu 8.
Mbali na hilo Chikota amezungumzia suala la sekta ya afya ambapo serikali ipo kuhakikisha inapunguza vifo vya mama na mtoto hivyo inaleta fedha kwa ajili ya ujenzi ya vituo vya afya katika kata mbalimbali kwenye halmashauri hiyo ikiwemo kata hiyo ya namtumbuka.



