Wananchi Ruvu Station wakosa huduma za afya

WANANCHI wa kijiji cha Ruvu Station Wilaya ya Kibaha Vijijini, mkoani Pwani wanakosa huduma za afya baada ya mradi wa ujenzi wa zahanati ya Ruvu Station kushindwa kumalizika kwa wakati kufuatia fedha zaidi ya Sh milioni 167 kufanyiwa ubadhirifu.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Iliyopo katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo amesema zahanati hiyo ilianza kujengwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Licha ya fedha hizo kutolewa ujenzi wake umekuwa ukisuasua kumalizika kwa bahadhi ya miundombinu ikiwemo, madirisha, milango na vyoo.

“Hakuna zahanati katika nchii iliyojegwa kwa gharama kubwa kama zahanati hii ya Ruvu station kuna fedha hapa zaidi ya milioni 167 zimefujwa na mpaka Sasa zahanati haijakamikika licha ya Halmashauri kutoa pesa nyingine jumla ya Sh milioni 51.”amesema Mwakamo

Aidha amesema baadhi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na halmashauri hiyo imekuwa ikikwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo usimamizi duni jambo ambalo limekuwa ni changamoto kwa wananchi.

“Nafurahi kuona kamati ya siasa Leo imekuja kutembelea mradi huu, watoa maamuzi ni ninyi na mmeona najua mtakuja na njia sahihi ya kudhibiti hali hii kwani utaratibu huo utasaidia miradi mingine kusimamia vema na kinachosumbua hapa ni fedha za walimu kufanyiwa ubadhirifu.”ameongeza

Awali akizungumza Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya hiyo, Bernad Ghaty amesema tayari chama hicho kilishatoa maagizo na kutoa muda wa siku 14 kwa halmashauri hiyo kumalizia ujenzi wa baadhi ya miundombinu jambo ambalo limepuuzwa mpaka Sasa.

“Kamati ya siasa imekuja hapa mara tatu na Sasa nasema hatua kuja tena hapa…maana tunakuja kila siku na tunaendelea kuwadanganya wananchi na wanakosa huduma za matibabu chama kilishanusa harufu ya ubadhirifu hapa.”amesema

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Vijijini, Edward Mshona alikiri kuwepo kwa changamoto hizo ikiwemo kushindwa kumalizika kujenzi wa zahanati hiyo Kwa  wakati na kwamba sababu kubwa ni kufungwa Kwa mfumo wa malipo serikali.

Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Mkali Kanusu amesema kamati ya siasa ya chama hicho imetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo baadhi yake imekuwa na changamoto ikiwemo zahanati hiyo na kwamba kikao cha Halmashauri Kuu kitakaa leo (kesho) na kuja na maazimio na maagizo.

Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo, Boniphas Boa amesema miundombinu ambayo bado haijakamikika ni madirisha 15,milango 17, matundu ya vyoo manne na mfumo wa majitaka na mfumo wa umeme.

Habari Zifananazo

Back to top button