Wananchi Same Magharibi wapewa taarifa njema

SAME, Kilimanjaro: KATIKA kipindi cha miaka mitano ijayo serikali imetenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi wa umeme ili uweze kuwafikia wananchi wa vitongoji vyote vya  Jimbo la Same Magharibi.

Hayo yalisemwa na Mgombea Ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk David Mathayo wakati akiomba ridhaa kwa wananchi wa Jimbo la Same Magharibi kumchagua kuendelea kuliongoza jimbo hilo katika sherehe ya uzinduzi wa kampeni ya ubunge na udiwani zilizofanyika katika Mji wa Hedaru Same.

Dk Mathayo alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imetumia mamilioni ya fedha kuhakikisha vitongoji vyote vya Jimbo la Same Magharibi vinapata umeme wa uhakika lakini ni vijiji vichache sana bado havijapata umeme ila miaka mitano ijayo vitakamilishwa ili kila mwananchi aweze kunufaika na nishati hiyo.

Alisema Rais amefanya mambo makubwa katika Jimbo la Same Magharibi mbali ya umeme pia huduma za miradi ya maendeleo kama vile afya ,maji, elimu na barabara mamilioni ya fedha yalipelekwa katika jimbo hilo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na yametekelezwa kwa vitendo.

Mathayo alisema huduma muhimu kama afya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imesogeza huduma hiyo karibu lengo ni kutaka wananchi kutosumbuka umbali mrefu kusaka huduma ya afya hivyo ni wajibu wake kuhakikisha kila fedha ya mradi iliyopelekwa na itakayoletwa katika Jimbo hilo inatumika ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema na kuwaomba wananchi wa Jimbo la Same Magharibi kumchagua mgombea Urais wa CCM,yeye kwa nafasi Ubunge kwa miaka mitano ijayo ikiwa ni pamoja na madiwani wa CCM ili aweze kutekeleza ipasavyo miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo iliyomalizika na iliyoanzishwa kwa miaka mitano ijayo.

‘’Nipeni kura nyingi mimi na mgombea wangu wa Urais ili tuweze kuendeleza pale nilipoishia juu ya miradi ya maendeleo kwani serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inawajali wananchi wa jimbo la Same Magharibu’’alisema Mathayo

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Same,Abdillah Suleiman kabla ya kumkabidhi ilani ya chama 2020/25 iliyotelekezwa na Ilani ya 2025/30 inayopaswa kutekelezwa na mgombea ubunge na madiwani alisema kuwa kila mmoja anapaswa kuwajibika katika kuitekeleza ilani hiyo kwa vitendo ili wananchi waendelee kuiamini serikali ya chama tawala.

Suleiman alisema  Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika miaka mitano iliyopita imefanya mambo makubwa katika Jimbo la Same Magharibi katika miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi ya afya,elimu,maji na barabara hivyo ni wajibu wa Mbunge na madiwani kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha za miradi hiyo ili iweze kutekelezwa na wananchi wafurahia maendeleo.

Alisema mamilioni ya fedha yaliletwa Wilaya ya Same hususani katika Jimbo la Same Magharibi kwa ajili ya miradi ya mendeleo hivyo ni wajibu wa Mbunge na Madiwani wataochaguliwa katika uchaguzi Mkuu ujao kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili wananchi waweze kuifurahia serikali yao miliyopo madarakani.

Naye Amri Mkwizu alisema kuwa CCM kupitia vikao vyake imefanya uteuzi madhubuti kwenye nafasi ya ubunge na udiwani kwani waliorudishwa kuwania nafasi hizo wote wana sifa stahiki za kuwaongoza wananchi kwani Chama kimezingatia maadili ,weledi ,uongozi bora na ushirikishaji.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button