DAR ES SALAAM: Halmashauri za Temeke na Kigamboni mkoani Dar es Salaam kupitia huduma ya Ardhi Kliniki zimetoa jumla ya hati 3700 wananchi wa halmashauri hizo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amesema hayo wakati akizindua Ardhi Kliniki katika Halmashauri ya Ubungo.
Amesema wananchi wa maeneo hayo wamepata hati hizo kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ya kupunguza gharama za kumiliki ardhi na uandaaji wa hati kwa asilimia 50 kupitia bajeti ya fedha ya mwaka 2023/24 Juni mwaka huu.
“Hii maana yake Rais Samia angependa watanzania wote wamiliki ardhi kwa kuwa na hati zao. Ni imani yangu kwa siku 25 tutakazokuwa hapa zitatatua matatizo ya ardhi ya wananchi wa Ubungo.
“Leo unaweza usijue umuhimu wa kumiliki ardhi na kuwa na hati kesho utakapoingia kwenye mgogoro ndipo utajua umuhimu wa kuwa na hati,” amesema.
Ameongeza kuwa wataanzisha mikoa mipya ya kiardhi ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam ili kupunguza uzito wa kazi kwa wataalamu wa mkoa na kumsogezea huduma mwananchi.
Kwa upande wake Paulo Kitosi kutoka Timu ya uratibu Mradi wa Uboreshaji Salama wa Milki za Ardhi amesema toka wameanza kazi hiyo mkoani Dar es Salaam Septemba 20 wameshasajili hati zaidi ya 3747 ambazo zilitolewa katika halmashauri ya Temeke na Kigamboni.
Amewataka wananchi walioko Halmashauri ya Ubungo na maeneo yote ya Dar es Salaam kufika katika eneo walilolitenga kwa ajili ya kutoa huduma hiyo kwa siku 25 katika halmashauri hiyo.
“Mwananchi akifika hapa ana uwezo wa kupata hati ndani ya siku moja,” amesema.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo Ardhi wa Ubungo, Fadhil Hussen amesema kupitia huduma hiyo wanaurasimishaji kwa kazi zilizokwama.
Amesema katika halmashauri hiyo kwa eneo hilo la Stop Over ambako wameanzia watakuwepo hapo kwa siku tano kisha watasogea eneo jingine.
Amesema katika halmashauri hiyo viwanja 6000 vina hati bado zaidi ya viwanja 20,000 hivyo aliwaalika wananchi wote kufika na kurasimisha ardhi zao.