Wanasiasa, wachumi Zanzibar wasifu bajeti

WANASIASA na wachumi wa sekta ya fedha zikiwemo benki, wameipongeza bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambayo inakwenda kujikita zaidi katika kuongeza vyanzo vya mapato pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano kwa Zanzibar kupata mgawo wa asilimia tisa katika misaada ya kibajeti.

Wakizungumza na gazeti hili baada ya kuwasilishwa kwa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Ofisa Mwandamizi wa Sera za Uchumi na Fedha wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Mohamed Hijja alisema bajeti imeweka kipaumbele katika kutumia mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato.

Alisema katika kuona serikali inakusanya mapato yake vizuri Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imepewa nguvu za kisheria kutekeleza majukumu yake katika sekta kodi hatua ambayo mapato yataongezeka.

Advertisement

“Nimefurahishwa na mikakati iliyowekwa na serikali katika kuiwezesha na kuipa nguvu Mamlaka ya Mapato ZRA katika kazi za ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vyote muhimu,” alisema Hijja. Mchumi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Kitengo cha Uchumi, Mohamed Hafidh alifurahishwa na bajeti ambayo sasa imeongeza kiwango cha fedha za misaada ya maendeleo ya kibajeti iliyokuwa ikipata Zanzibar kutoka asilimia 4.5 ya zamani hadi kufikia asilimia tisa.

Alisema marekebisho hayo yanaonesha nia ya dhati iliyopo kwa viongozi wakuu wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano, ambako kiwango cha asilimia 4.5 kilikuwa kikilalamikiwa muda mrefu na Zanzibar na kuomba kifanyiwe marekebisho.

Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said alisema ni bajeti inayokwenda na mahitaji ya matakwa ya wananchi katika kutoa fursa za kiuchumi na ujasiriamali. Kwa mfano, alisema miongoni mwa ahadi za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ni kukuza na kuimarisha uwekezaji katika uchumi wa buluu ikiwamo mazao ya baharini yanayotokana na mwani na matango bahari.

Mwakilishi wa Kuteuliwa na Rais, Juma Ali Khatib alipongeza bajeti hiyo aliyosema imeonesha nia ya viongozi wote katika kuimarisha Muungano na kuzipatia ufumbuzi kero zake. Naye Mwakilishi wa Jimbo la Bumbwini, Mtumwa Peya Yussuf alisema bajeti imeweka kipaumbele kwa jamii ya wanawake wajasiriamali kuona wanapiga hatua kubwa ya maendeleo na kujikomboa kiuchumi.

Ofisa Mwandamizi wa ZRA, Hafidh Ussi alisema wamejipanga kuhakikisha vyanzo vyote vilivyokuwa vikivujisha mapato vinadhibitiwa ikiwamo matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki katika taasisi zote. Naye Ofisa Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ofisi ya Zanzibar ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kufikiwa kwa kiwango cha asilimia tisa kwa kiasi kikubwa kutaongeza kiwango cha mgawo unaopata Zanzibar katika sekta mbalimbali ikiwamo Benki Kuu.

Alisema hatua hiyo itaiwezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Tume ya Pamoja ya Fedha kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na mgawo wa Serikali ya Muungano katika fedha za misaada ya kibajeti.