SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Dodoma limewataka wananchi wa vijijini kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa bei nafuu pindi huduma hiyo inapofika kwenye maeneo yao.
Rai hiyo ilitolewa na Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Dodoma, Sarah Libogom wakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa wananchi.
Tanesco Mkoa wa Dodoma imekuwa ikitoa elimu na uhamasishaji katika vijiji vinavyonufaika na miradi ya umeme ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inayoendelea wilayani Kondoa.
Elimu hiyo kwa umma imehusisha kuelimisha wananchi juu ya miradi ya REA na utekelezaji wake, uepukaji vishoka pamoja na matumizi sahihi ya umeme wenyewe ikiwemo uzingatiaji wa usalama kwanza.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kikilokati, Berabera na Kwahengwa, aliwataka wananchi kuhakikisha wanapokea miradi ya umeme inayoendelea kwenye maeneo yao kwa kuhakikisha wote waliofikiwa na nishati hiyo wanajitokeza kuomba kuunganishwa kwenye huduma kupitia Mfumo wa NiKONEKT.
“Wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hii kupitia mfumo wa NiKONEKT kwa kutumia simu zao, mfumo ambao ni rahisi na una ufanisi zaidi hasa kutokana na serikali kupunguza gharama kwa wananchi,” alisema na kuongeza:
“Kwa Sh 27,000 unakuwa umepata huduma kwa fedha ambayo unaweza kuzipata kwa kuuza kuku wawili na unaunganisha huduma ya umeme milele kwenye nyumba yako, hivyo ni vyema kuhakikisha unatumia fursa hii vizuri kwani umeshawashwa na mradi upo ukingoni kukamilika.”
Pia aliwahimiza wananchi kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza kipindi chote cha mradi na kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka za serikali zilizopo katika maeneo yao.
Alisema wananchi pia wanapaswa kuzingatia usalama katika matumizi ya umeme ikiwamo kutofanya shughuli zozote chini au karibu na miundombinu ya umeme kama vile transfoma.
“Pia hakikisheni mnawatumia mafundi wanaotambulika katika utandazaji wa nyaya za umeme katika nyumba zenu pamoja na kutokata miti iliyo karibu na nyaya za umeme bila kushirikiana na uongozi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Kikilo, Yuda Daniel aliishukuru serikali kwa kupeleka miradi hiyo kwa kuwa kilikuwa kilio kikubwa kwa wananchi wapate umeme huku akisisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili kufanikisha miradi hiyo.
“Wananchi wana matumaini makubwa na serikali yao hivyo naamini watatoa ushirikiano wa kutosha kwani wamefurahia kufikiwa na mradi huu,” alisema.
Kwa nyakati tofauti wananchi wameishukuru serikali kusogeza huduma ya umeme na kuiomba kuendelea kufikiwa kwa vile vitongoji ambavyo bado navyo serikali ivikumbuke.
Uhamasishaji huo umefanywa na Tanesco kwa kushirikiana na Mkandarasi Ok Electrical anayetekeleza mradi huo kwenye vijiji 72 vya wilaya za Kondoa na Mpwapwa ambaye hadi sasa ameshatekeleza takribani asilimia 50 ya mradi huo.
Mradi huu unatarajia kumalizika January 2023, ambapo katika Wilaya ya Kondoa pekee vijiji 14 kati ya vijiji 34 vimewashwa, huku kazi ya kuwasha ikiendelea katika vijiji 20 vilivyobakia.