DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Maybelline NewYork imetangaza programu ya mafunzo kwa wanawake 1,000 wa Tanzania katika sanaa ya urembo wa kitaalamu unaotarajia kuanza miezi mitatu ijayo.
Kutangazwa kwa mpango huu kumeenda sanjari na kuingia rasmi kwa bidhaa za urembo zinazozalishwa na Maybelline katika soko la Tanzania, unaolenga kuwapa wanawake ujuzi ambao utafungua milango ya ajira na ujasiriamali katika sekta ya urembo.
Akizungumza Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bidhaa hizo Victoria Karanja, Meneja Mkuu wa Bidhaa za Watumiaji wa kampuni hiyo amesema kuwa Maybelline NewYork ni zaidi ya vipodozi, bali pia ni mapinduzi ya kiuchumi kwa wanawake na wasichana wa Tanzania.
Amesema programu hiyo inatarajiwa kuleta fursa mpya za kiuchumi, kuwezesha wanawake kuanzisha biashara zao wenyewe au kupata kazi katika saluni, bidhaa za urembo na sekta ya burudani.
“Kwa kujifunza mbinu za urembo wa kitaalamu, washiriki hawataongeza tu uwezo wao wa kupata mapato, bali pia watachangia ukuaji wa sekta ya urembo nchini Tanzania,”amelngeza.
Karanja amesema kuwa mafunzo hayo yataongozwa na wasanii wa urembo wenye majina makubwa wa ndani na nje ya nchi ambao watawafundisha washiriki mbinu za hali ya juu, mikakati ya biashara na ujuzi wa bidhaa ili kuwasaidia kujenga kazi zenye mafanikio.