Wanawake Kagera wapewa uwezo fursa za uvuvi

ZAIDI ya vikundi 100 vya wanawake wanaoishi kando ya visiwa vya Ziwa Victoria mkoani Kagera wameendelea kujengewa uwezo kupitia mashirika ya EMEDO na WORDFISH namna ya kutumia fursa za uvuvi.

Katika kikao cha tathmini na mafunzo endelevu namna ya kutumia fursa za serikali kuhusu mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri, baadhi ya wanawake kutoka vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na uvuvi na uchakataji wa dagaa wameeleza namna walivyoanza kunufaika.

Jovitha Chrizostom kutoka Wilaya ya Muleba amesema hivi karibuni mashirika yaliwapa mafunzo namna ya kuangalia fursa wanazoweza kunufaika nazo katika uvuvi na kwa sasa wanajishughulisha na kuchakata dagaa na kujipatia kipato.

Advertisement

“Kikundi chetu kina wanawake 12 baada ya mafunzo ya kutumia fursa zilizotuzunguka kisiwani tuliona tunaweza kuchakata dagaa, lakini hofu ilikuwa tutasogelea vipi boti za wavuvi tulianza hivyo hivyo kwa kulazimisha mpaka sasa tumeondoa mila potofu EMEDO wametujengea nyavu,” amesema Chrizostom.

Jeniva Kanganyira kutoka kijiji cha Rwazi kikundi cha urafiki ambacho kinamiliki mitumbwi ya uvuvi kutoka Mwalo wa Rwazi  amesema halikuwa jambo raisi kumiliki mitumbwi ikiwa wao ni wanawake ila wameendelea kuelimishwa . Amesema kwa sasa wanamiliki mitumbwi yao bila changamoto na wanapata kipato kutokana na kuvua samaki.

Mwakilishi wa Meneja wa Shirika la EMEDO,  Ilucyphine Kilanga amesema mpaka sasa wameendelea kutoa elimu ya kujipatia kipato kwa vikundi vya wanawake katika visiwa vya Ziwa Victoria mkoani Kagera, kuweka miundombinu ya kuanika na kuchakata dagaa, kutoa vifaa kwa wanawake wanaoweza kukaanga dagaa vizuri.

“Shirika letu lilifanya utafiti na kubaini kuwa kuna mila kandamizi kwa wanawake ambao  wamengukwa na fursa lukuki katika maswala ya uvuvi kwa mfano wanawake hawakuwa huru kumiliki boti,kuchakata dagaa ,kuuza wenyewe, kuchukua mikopo kwa uhuru kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la WORDFISH tunaona mabadiliko makubwa sana kwa vikundi vya wanawake,”amesema Kilanga.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba, Edna Kabyazi ametoa shukurani kwa mashirika ambayo yameendelea kuungam mkono juhudi za serikali juu ya mila kandamizi na kudai kuwa uwepo wa vikundi imara  vya wanawake wanaojihusisha na maswala ya uvuvi imewarahisishia wilaya hiyo kubaini kwa urahisi namna wanavyoweza kutumia mikopo ya Halmashauri kuinua uchumi wao huku akidai kuwa kiasi cha Sh bilioni 1.7 kinawasubiri kama mikopo .