Wanawake Missenyi wasifu kuondokana na mila kandamizi

BAADHI ya wanawake wa kijiji cha Katendaguro kata Bugandika wilayani Missenyi mkoani Kagera wameipongeza Kampeini ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa kutuma wataalamu kutoa mafunzo ya kisheria yanayolenga kuwaondoa wanawake katika mila potofu hasa urithi wa mali.

Mmoja wa wanawake mwenye umri wa miaka 70 ambaye tayari amempoteza mme wake aliwakilisha shitaka lake mbele ya wataalamu kuwa miaka 40 sasa tangu alipofiwa na mme wake lakini mtoto wake aliyeandikwa kama mrithi amekuwa akikinzana kumtoa katika nyumba ya mmewe hali ambayo inamfanya kuishi na wasiwasi.

“Nimezaa na mme wangu ,tumechuma mali ,tumepata watoto wa kike na huyu wa kiume wa mwisho , na katika wosia mme wangu alimrithisha lakini sasa sina raha mtoto wangu wa kumuzaa anasema yeye  amerithishwa mimi niondoke  niende kwetu najiuliza nitaendaje kwetu wakati nimezeeka na mme amekufa na tumetafuta mali pamoja,natumaini nitapata msaada kupitia kampeini hiyo, “amesema.

Agnes Ernest mkazi wa kijiji hicho alisema wanawake wa kijiji hicho wameipokea kampeini hiyo mikono miwili kwani wanawake wengi wanapitia maumivu makali sana hasa wanapofiwa na wanaume zao huku wazazi waliozaa mabinti wakigubikwa na sintofahamu  na hawajui ipi itakuwa hatima ya mabinti wao mara watakapofariki hasa katika swala la kuwarithisha

Moja ya elimu iliyotolewa na mjumbe wa kamati ya uratibu wa kampeini hiyo wakili wa kujitegemea    Jofrey Binamungu alisema kijiji icho ni miongoni mwa vijiji vinavyogubikwa na maswala ya mila na desturi  mbaya ambazo zinawakandamiza wanawake juu ya kumiliki na kurithi mali huku akidai kuwa nyumba inayomilikiwa na mme na mke inapaswa kuwa ya kati ya mke na mme endapo mmoja akifa bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Alisema kuwa kampeini ya kisheria imeletwa mahususi kutoa elimu kwa wananchi wote  wa Wilaya ya Missenyi na Mkoa wa Kagera kwa ujumla kuwa kuzaa binti sio kosa na kufiwa na mme sio kosa kwani wanaume na wanawake wanahaki ya kupata mali na kuandikwa vizuri katika mirathi.

Deodatus Rweyemamu 61 mkazi wa Katendaguro ambaye amefanikiwa kupata uzao wa mabinti 5 ameopongeza kampeini hiyo Kwa kumuondolea Dukuduku kwani alikuwa anawaza ni kwa jinsi Gani Ataandika wosia juu ya mabinti zake kupewa mali kwani hakubahatika kupata mtoto wa kiume ambaye wengi wanamchukulia kama mrithi  na kumutupa Kando mtoto wa kike.

“Kampeini imeniondolea Dukuduku sasa naweza kujisikia vizuri, kwa kupata elimu juu ya namna ya kuwakabidhi mabinti mali zangu mali kwa sababu hali ya sasa ndugu anaweza kugeuka, pamoja na kuwa wenye malalamiko leo ni wanawake lakini hata sisi wanaume tuliozaa mabinti tunajisikia vibaya, hongera sana kwa Rais,”amesema Rweyemamu.

Mratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria wilayani Missenyi Maxmillan Fransis alisema kuwa moja ya changamoto kubwa za kisheria zilizojitokeza na kuendelea kutafutiwa ufumbuzi na wataalumu ni maswala ya wanawake ambao wameshindwa kupata mali zao kisheria  na wamebaki kuwa wapangaji katika maeneo yao halali huku akisema kuwa hata kampeini hiyo hata ikiisha bado elimu ya kisheria itaendelea kutolewa na  maafisa dawati ambao wameajiliwa kupitia kampeini hii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button