‘Wanawake wanataaluma ombeni kwa ajili ya Taifa’

MKE wa Waziri Mkuu msaafu, Jaji Joseph Warioba,  Evelyne  Warioba, amewataka wanawake wanataaluma kumuomba Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Taifa.

Amesema ufumbuzi unapatikana kwa Mungu na viongozi wanawake waangalie la kufanya, ikiwemo matatizo makubwa yanayowakumba wanawake na watoto.

Ametoa kauli hiyo Dar es Salaam leo, katika maombi maalum  ya wanawake wanataaluma yaliloandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya uwezeshaji wanawake na vijana kufikia malengo (YLPT), ili kuombea Taifa katika matukio mbalimbali.

Kuhusu wanawake wanataaluma, amesema  matatizo makubwa ya vijana vyanzo vyake ni kwenye jamii na wanawake wanataaluma wana mchango wa kunyanyua vipaji vilivyo ndani ya kundi hilo.

Mama Warioba amesema ni wajibu wa wanawake wanataaluma kuomba kwa Mungu kwa ajili ya nchi na viongozi waliomo, ili mipango na mikakati inayopangwa iwe na mafanikio kwa jamii.

“Mara nyingi hatutaki kutumia kile tulichopewa na Mungu kwa ajili ya wengine, labda kwa kuona aibu kwa utaalam tulionao ni vyema kuamka sasa, jambo litakalosaidia kuponya kuanzia ngazi ya familia,” amesema Mama Warioba.

Naye Mkurugenzi wa  YLPT, Grace  Masalakulangwa, amesema miongoni wanataaluma hao wanaomba kwa Mungu ni pamoja na tathmini ya sensa kuwa na majibu chanya, kuombea serikali na mihimili yake mikuu pamoja na vijana na wanawake waweze kutimiza malengo yao.

Amesema wanawake wanataaluma wanayo nafasi kubwa kurudisha kile walichokipata katika elimu na utumishi pia na kupitia maombi, watasaidia jamii kwa namna moja hadi nyingine.

Amesema kuna haja ya  kuombea majibu ya sensa, ili wanaofanya kazi hiyo waifanye kwa weledi, jambo litakalosaidia nchi kufikia malengo ya maendeleo.

” Ni muhimu kwa wanawake wanataaluma kuomba kwa ajili ya Taifa, ili popote wanawake walipo kwenye utumishi  na hata katika biashara kutumia taaluma zao kwa uadilifu  na kuisaidia nchi kwa namna moja hadi nyingine,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button