Wanawake watakiwa nafasi za juu NCAA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk, Pindi Chana amesisitiza Mamlaka ya (NCAA ) inapaswa kuongeza jicho katika kuhakikisha wanawake wanafikia nafasi za juu za uongozi katika nafasi mbalimbali.
Dk, Chana ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa kuwavisha cheo manaibu kamisha wawili huku makamishna wasaidizi waandamizi watano wakivishwa vyeo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NCAA, Jenerali Mstaafu,Venance Mabeyo.
Amesema kijeshi ni tafsiri ya kupanda cheo na ukipanda cheo ujue unamajukumu ya kiuongozi hivyo maofisa hao wanajukumu kubwa la kusimamia shughuli za uhifadhi, maendeleo ya jamii na urithi wa utamaduni na utalii.
Alisisitiza NCAA kuangalia namna ya kuongeza ushiriki zaidi wa wanawakeji katika nafasi mbalimbali za uongozi na kusisitiza rasilimali zilizopo kutunzwa na kulindwa zaidi ikiwemo wananchi kupewa elimu zaidi ya kulinda wanyamapori
“Angalieni namna ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na nafasi za juu pia wawepo lakini serikali kupitia Rais Samia Hassan Suluhu imefanya mengi katika sekta ya utalii ikiwemo kulinda maliasili zilizopo katika kukuza uchumi”
Huku Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA,Jenerali Mstaafu Mabeyo aliwavisha vyeo makamishna wengine ambao ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia idara ya Mipango na uwekezaji, Gasper Lyimo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Paul Shaidi anayesimamia Kitengo cha huduma za Sheria, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Charles Wangwe anayesimamia Idara ya Uhasibu na fedha.
“Mafanikio ya Ngorongoro yanategemea uadilifu na uwezo wa viongozi wake na kuwaasa viongozi waliovishwa vyeo kubeba matumaini mapya katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii lakini pia nampongeza Balozi Chana, serikali kwa ujumla na wadau wa utalii kwa kuiunga mkono Ngorongoro na hatimae kutangazwa kama Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika kwa mwaka 2025.
Wakati huo huo, Kamishna wa Uhifadhi (NCAA) Abdul-Razak Badru amesema NCAA imedhamiria kuboresha miundombinu katika eneo la Ngorongoro ikiwemo barabara, vituo vya ulinzi , usaidizi, watoa taarifa, malazi ya watalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha inakuwa bora zaidi na kuvutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani na nchini.