Wanne wadaiwa kufa moto mganga akiwaondolea mikosi

WATOTO wanne wamefariki dunia baada ya kuungua na wengine saba kujeruhiwa kwa moto uliowashwa kwa madai ya kuondoa mkosi katika familia.

Vifo hivyo vilitokea usiku wa kuamkia jumatano katika Kijiji cha Magili Juu, Kata ya Kigwa wilayani Uyui mkoani Tabora na moto huo unasadikiwa kuwa uliwashwa na mganga aliyekuwa amekwenda kuwaondolea mkosi.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alithibitisha tukio hilo na kusema mganga anayetuhumiwa kuhusika amekamatwa na kwamba upelelezi wa tukio hilo unaendelea.

Advertisement

Akieleza undani wa tukio hilo, Diwani wa Kata ya Kigwa, Bakari Kabata alieleza kuwa mkuu wa kaya alimuita mganga wa kienyeji kwenda kuondoa mkosi kwenye familia hiyo.

Kwa mujibu wa Kabata, mganga aliagiza kitengenezwe kibanda cha nyasi na kuwaambia waingie ndani ili akiwashe moto na wao watoke nje mmoja baada ya mwingine.

Alisema moto huo ulizidi kisha kusababisha watu hao wanne kupoteza maisha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magili Juu, Said Magari alitaja waliofariki kuwa ni Kashindye Machia (5), Shija Samwel (5), Dotto Masasi (3) na Jeremia Samwel (7).

Waliojeruhiwa ni Samwel Masasi (40), Sida Samwel (10), Masasi Samwel na Dotto Machia (wote miaka 9), Shija Samwel miaka (7), Halima Samwel (11) na Regina Masanja (65).