Wanne wadakwa na vito vya mil 54/-

WATU wanne wamekamatwa na madini ya vito katika Mtaa wa Togo, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.Watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni iliyofanywa na Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi Mahenge kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Ulanga na uongozi wa wilaya hiyo.

Ofisa Madini Mkazi Mahenge, Jonas Mwano amesema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya taarifa za kiintelijensia kuonesha kulikuwa na biashara ya madini inayofanyika kinyume cha sheria katika makazi ya watu. Mwano amewaambia waandishi wa habari kuwa  hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha rasilimali za madini zinalindwa na kunufaisha taifa kupitia mfumo rasmi wa masoko.

Watuhumiwa hao wamekamatwa na madini mbalimbali yakiwemo spineli, rodolaiti, tuarmalini na glasi ya vilkano. Madini hayo yalipatikana nyumbani kwa mmoja wao ambaye pia alikutwa akifanya usanifu wa madini bila kuwa na leseni ya usanifu wa madini kinyume cha Sheria ya Madini Sura 123.

Mwano amesema watuhumiwa walifikishwa katika Kituo cha Polisi Mahenge na kufunguliwa jalada la uchunguzi MHE/ IR/1189/2025 na madini yote yalifanyiwa uthamini kubaini uzito, aina, ubora na thamani yake.

Amesema madini hayo yana thamani ya Sh milioni 54.02 na serikali ilitarajia kukusanya zaidi ya Sh milioni 5.05 kupitia kodi na tozo za madini hayo. Mwano amesema shughuli za usanifu wa madini zinaruhusiwa kwa mtu mwenye leseni ya usanifu wa madini ambayo hulipiwa Sh 2,930,256 sawa na Dola za Marekani 1,200 kwa mwaka.

Amesema kukiuka matakwa hayo ni kwenda kinyume cha sheria na mfanyabiashara yeyote hatapewa nafasi kufanya shughuli hizo bila vibali. SOMA: Rukwa yawavutia wawekezaji kimataifa sekta ya madini

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button