Wanodhalilisha watoto kwa maudhui mitandaoni wasichekewe

SERIKALI kupitia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dorothy Gwajima imelaani vitendo vya baadhi ya watu kuwatumia watoto kuandaa maudhui yasiyofaa kwenye mitandao kinyume na sheria.
Vilevile imelaani vitendo vya baadhi ya watu wasiokuwa na vibali kisheria wala taaluma ya kuandaa maudhui yenye tija mitandaoni na kusambaza maudhui hayo kinyume na sheria ya mitandao, hivyo kuathiri watumiaji wa maudhui hayo na kusababisha mmomonyoko wa maadili na kudhalilisha watoto.
Katika taarifa yake Dk Gwajima alitoa mfano kuhusu kinyozi anayelalamikiwa kwa maudhui yake katika mitandao ya kijamii kuwa imevuka mipaka ya kazi yake kwa kudaiwa kuchukua watoto na kuwafundisha mada zinazohusu kufanya mapenzi na watu wakubwa na kuzisambaza mitandaoni.
Nasi tunaungana na serikali kulaani vitendo hivi vya kudhalilisha watoto mitandaoni kwa madai ya kutengeneza maudhui kufurahisha watu au watumiaji wa mitandao hiyo.
Ni kweli tabia ya baadhi ya watu kutumia watoto katika mitandao kuandaa maudhui mbalimbali, yakiwemo yasiyofaa imekuwa ikikithiri ilihali ni ukiukaji wa Sheria ya Mtoto Sura ya 13.
Mitandao ya kijamii siku hizi imegeuzwa kuwa lango la mafunzo mabaya kwa watoto hasa kutokana na baadhi ya watu wasiokuwa na maadili wala aibu kuitumia teknolojia vibaya.
Tunaamini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa na serikali na jamii kwa ujumla kuelimishana, kuonyana na kukemeana pale baadhi wasiojielewa wanapotumia mitandao vibaya kwa kurubuni na kushirikisha watoto katika maudhui ya hovyo, yakiwemo ya kingono au kutumikisha watoto kwenye vitendo hivyo.
Matumaini yetu serikali itaendelea kuwadhibiti zaidi na kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya watakaobainika kukiuka haki za watoto kwa kuwadhalilisha mitandaoni kwani vitendo hivyo ni makosa ya jinai na watumike kama mfano kwa wale wote wasiothamini utu wa watoto.
Tunaikumbusha jamii kuwa mitandao ya kijamii huhifadhi vitu na maudhui, kama mtoto au watoto watatumika kwenye maudhui yasiyofaa yanaweza kuja kutumika katika maisha yao ya baadaye na kusababisha madhara katika maisha yao, ikiwemo utu wao.
Tunaamini ni wajibu wa kila mpenda maendeleo na teknolojia kuheshimu utu wa mwingine hususani kuwalinda watoto wasigeuzwe kuwa waathirika wa matumizi mabaya ya maudhui ya mitandao ya kijamii.
Sheria ziheshimiwe, watoto wathaminiwe na sheria zifuatwe na hatua stahiki zichukuliwe pale sheria, kanuni na taratibu za nchi zilizowekwa zinapokiukwa ili tuwe na jamii iliyojengwa katika nidhamu, maadili mema na hofu ya Mungu.